TANZANIA NA AUSTRIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA KIJAMII KUPITIA MKAKATI MPYA WA ‘AUSTRIA-AFRICA 2026–2029’.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Austria ili kuhakikisha kuwa malengo ya Mkakati mpya wa Austria-Africa wa mwaka 2026 hadi 2029 yanafikiwa kama yalivyopangwa. Mhe. Munde alisema hayo alipokutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Hannah Liko, katika kikao kilichojadili masuala ya mkakati wa Austria wa kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ikiwemo ushirikiano katika kukuza uchumi kati ya Austria na Tanzania, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam. Alisema kuwa Mkakati huo mpya wa Austria-Africa wa mwaka 2026 hadi 2029 umejikita katika maeneo makuu manne ambayo ni amani na usalama, ushirikiano wa kiuchumi, uhamiaji, pamoja na elimu na sayansi.