TANZANIA KUJENGA KITUO CHA UMAHILI CHA HUDUMA YA MATIBABU
Tanzania inatarajiwa kuwa miongoni mwa nchi tano za Afrika zitakazonufaika na ujenzi wa mradi mkubwa wa Hospitali itakayokuwa na viwango vya dunia vya utoaji huduma za matibabu (African Medical Center of Excellence (AMCE), kupitia mradi unaotekelezwa na African Export-Import Bank (Afreximbank) kwa kushirikiana na Hospitali ya Chuo Kikuu cha King, iliyoko London nchini Uingereza.
Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Umahili cha Kimatibabu, Abuja, Bw. Brian Deaver, wakati Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipoongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea ujenzi wa mradi wa aina hiyo, nje kidogo ya mji wa Abuja, nchini Nigeria.