SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA TAKWIMU BORA KATIKA USIMAMIZI WA UCHUMI

Serikali imesisitiza umuhimu wa matumizi ya takwimu sahihi na zenye ubora katika kusimamia uchumi wa Taifa, kwa kuwa taarifa hizo ni msingi wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu mipango ya maendeleo, matumizi ya fedha za umma na uwekezaji katika sekta mbalimbali. Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 12 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.