MHE. MUNDE: UWEKEZAJI NA MAENDELEO LAZIMA VIENDE SAMBAMBA NA MABADILIKO YA TABIANCHI.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa wawekezaji wa kimataifa na taasisi za fedha za maendeleo kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini, ikisisitiza kuwa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lazima ziendane na mabadiliko ya kiuchumi na uboreshaji wa maisha ya wananchi.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, baada ya Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Jukwaa la Kimataifa la Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi (Private Climate Finance Community), uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, Marekani ikiwa ni sehemu ya Mikutano ya Athari za Maendeleo Endelevu 2026 (SDIM26) inayoendeshwa na Baraza la Uchumi la Dunia (WEF).
