JAPAN YAIPIGA JEKI TANZANIA UJENZI WA BARABARA ZA MZUNGUKO JIJINI DODOMA

Japan, kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA), imeipatia Tanzania msaada wa yen bilioni 4.07 sawa na shilingi bilioni 68.5 za Tanzania kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa Barabara ya mzunguko wa ndani katika Jiji la Dodoma. Mkataba wa Msaada huo umetiwa Saini katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa upande wa Tanzania, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yasushi Misawa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), Hitoshi Ara. Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema kuwa Mradi huo utahusisha upanuzi wa barabara kutoka njia mbili hadi nne kuanzia mzunguko wa barabara ya Bahi hadi Image na ujenzi wa barabara mpya ya njia nne kuanzia mzunguko wa barabara ya Image hadi mzunguko wa barabara ya Makulu.