IMF YAIPONGEZA TANZANIA KWA USHIRIKIANO NA USIMAMIZI MZURI WA ECF NA RSF.

Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, limeipongeza Tanzania kwa ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Shirika hilo katika utekelezaji na usimamizi wa mageuzi ya kiuchumi chini ya programu za Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii na Resilience Sustainability Facility (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Pongezi hizo zimetolewa na Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Nicolas Blancher, wakati alipoongoza timu ya wataalamu kutoka Shirika hilo iliyofika kufanya tathmini ya kina ya program mbalimbali inayofadhili nchini, katika kikao na Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.