DKT. MWAMBA AJADILI UFADHILI KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ametoa wito kwa Benki Kuu za Nchi za Afrika, kuweka mipango na mikakati ya kutafuta fedha kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo sekta binafsi kwa ajili ya kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi katika nchi hizo.
Dkt. Mwamba ametoa rai hiyo wakati akishiriki mjadala kuhusu wajibu wa Benki Kuu za nchi za Afrika kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Macroeconomic and Financial Management of Eastern and Southern Africa (MEFMI), mjadala uliofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), katika Hoteli ya Mayflower, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.