BI. OMOLO ASISITIZA WAKAGUZI WA NDANI KUZINGATIA UADILIFU KATIKA UTENDAJI KAZI.

Watumishi wa Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali wamehimizwa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kujituma kwa kuwa ni daraja muhimu kati ya usimamizi wa fedha za umma na mafanikio ya maendeleo ya wananchi. Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Huduma za Hazina, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, wakati akifungua Mkutano wa Watumishi wa Idara hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Olasite Garden, jijini Arusha. Alisema mkaguzi wa ndani si tu mtathmini wa taarifa za kifedha, bali ni mshauri wa usimamizi bora, anayechangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha taasisi zinafanya kazi kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya sheria, taratibu na kanuni.