Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WIZARA YA FEDHA YAAGIZA TAASISI ZILIZOISABABISHIA SERIKALI HASARA YA BILL. 8.7 KUCHUKULIWA HATUA

29 Sep, 2023
WIZARA YA FEDHA YAAGIZA TAASISI ZILIZOISABABISHIA SERIKALI HASARA YA BILL. 8.7 KUCHUKULIWA HATUA

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akipokea ripoti ya tathmini ya utendaji kwa mwaka wa fedha 2022/23 ya Taasisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi hiyo, Dkt. Leonada Mwagike, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Hazina, jijini Dodoma.Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Bw. Eliakim Maswi.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) ameziagiza Mamlaka zote zinazohusika na makosa ya jinai hususan Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuzichukulia hatua kali za kisheria Taasisi 12 za umma zilizoisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 8.77.

Alitoa agizo hilo jijini Dodoma baada ya kupokea Ripoti ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Mhe. Chande alisema ripoti hiyo imebainisha kuwa Serikali ilipata hasara hiyo kutokana na ukosefu wa uwajibikaji, ufanisi, uwazi na uadilifu katika Taasisi 12 zilizochunguzwa.

“Vitendo hivi ni vya jinai vinavyohujumu uchumi wa nchi na hivyo hatua kali hazina budi kuchukuliwa kwa wahusika wote”, alisisitiza Mhe. Chande.

Alisema Serikali haitavumilia Taasisi zinazokiuka Sheria, Kanuni na Miongozo ya ununuzi wa umma na kurudisha nyuma juhudi za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

“Mamlaka ilifanya ufuatiliaji kuhusu matumizi ya mfumo wa TANePS ambapo matokeo yalibainisha kuwa Taasisi 132 kati ya 864 hazikutumia mfumo katika ununuzi wao. Kitendo hiki ni ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na maelekezo ya Serikali”, aliselima Mhe. Chande.

Alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali kusimamia na kulifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha taasisi nunuzi zote za Serikali kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 2 wa mwaka 2023/24, kwa kuhakikisha zinafanya ununuzi wa umma kupitia mfumo wa NeST kuanzia tarehe 1 Oktoba 2023. 

Aidha, aliipongeza PPRA kwa uchunguzi na ukaguzi maalum ulioufanya na kuiwezesha Serikali kuokoa fedha za umma ambazo zitaenda kutumika katika kuleta maendeleo ya nchi na kutoa huduma kwa watanzania kama vile ujenzi wa vituo vya afya na madarasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dkt. Leonada Mwagike alisema Mamlaka hiyo ilifanya ukaguzi kwa Taasisi nunuzi 180 ikihusisha Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Mashirika ya Umma.

Alisema katika matokeo ya ukaguzi huo yanaonesha kuwa kati ya Taasisi 180 zilizokaguliwa Taasisi 28 zilikuwa na matokea ya kuridhisha, 109 zilikuwa na matokeo ya wastani na taasisi 43 zilikuwa na matokeo hafifu.

“Kati ya Taasisi 43 zilizopata matokeo hafifu Taasisi 28 zilikuwa kwenye kundi la Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, 8 zilikuwa kwenye kundi la Mashirika ya Umma na Taasisi 7 zilikuwa kwenye kundi la Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Wakala wa Serikali”, Alibainisha Dkt. Mwagike.

Zoezi la kukabidhi ripoti hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ambayo inaitaka PPRA ndani ya miezi mitatu baada ya mwaka wa fedha kumalizika kutoa taarifa ya utendajikazi na tathmini utendaji kwa mwaka uliopita.

Mwisho.