Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WAZIRI WA FEDHA AZINDUA HARAMBEE, AWATAKA WANANCHI KUENZI MCHANGO WA MASHEIKH WALIOTANGULIA MBELE YA HAKI

16 Mar, 2026
WAZIRI WA FEDHA AZINDUA HARAMBEE, AWATAKA WANANCHI KUENZI MCHANGO WA MASHEIKH WALIOTANGULIA MBELE YA HAKI

Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewataka waumini wa dini ya kiislam kuendelea kuenzi mchango wa viongozi wa dini waliotangulia mbele ya haki kwa kudumisha maadili, mshikamano na amani katika jamii.

Waziri Balozi Omar alitoa wito huo alipokuwa Mgeni Rasmi katika dua na harambee ya kuwaombea Masheikh waliotangulia mbele ya haki iliyofanyika Buguruni Malapa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa dini, Serikali na wananchi wa Buguruni, Mhe. Balozi Omar alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha washiriki kukutana katika mkusanyiko huo wa kheri wa kuwaombea Masheikh, wazazi na ndugu waliotangulia mbele ya haki.

Katika hotuba yake, alimpongeza Diwani wa Kata ya Buguruni, Mheshimiwa Zahoro Muhaji, kwa uongozi wake na kwa kuendelea kuhamasisha shughuli zinazojenga mshikamano wa jamii pamoja na kuheshimu na kuenzi mchango wa viongozi wa dini.

“Tukio kama hili ni ishara ya uongozi wenye busara unaojali maadili ya jamii na kuthamini mchango wa wale waliotutangulia,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Alisema Uislamu unafundisha kuwa dua za walio hai zina manufaa kwa waliotangulia mbele ya haki, akisisitiza kuwa dua hizo ni sehemu ya kuwakumbuka kwa wema wale waliowalea kiroho na kuwafundisha maadili.

Mhe. Balozi Omar alisema Masheikh waliotangulia walikuwa taa ya mwanga katika jamii kwa kuwa walitoa elimu ya dini, walikuwa wapatanishi wa migogoro na walezi wa kizazi.

Aidha, aliwakumbusha wananchi kuwa maisha ya duniani ni ya muda mfupi na kwamba mema yanayofanywa kwa ajili ya jamii ndiyo hubaki kama kumbukumbu njema.

Katika hafla hiyo, Mhe. Balozi Omar pia alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuthamini mchango wa taasisi za dini katika kujenga maadili ya jamii, kuimarisha umoja wa Watanzania na kulinda amani ya taifa.

Sambamba na hilo, Mhe. Balozi Omar alizindua rasmi harambee iliyolenga kusaidia shughuli za kidini na kijamii na maendeleo ya jamii ya Buguruni.

Alisema harambee hiyo inaonesha moyo wa kusaidiana na kujali ustawi wa jamii, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, viongozi na wananchi kuchangia kwa moyo wa ukarimu ili kufanikisha lengo hilo.

Kwa upande wao, Diwani wa Kata ya Buguruni, Mheshimiwa Zahoro Muhaji na Sheikh wa Wialaya ya Ilala, Sheikh Adam Mwinyipingu, walisisituiza umuhimu wa maadili mema kwa makundi mbalimbaloi pamoja na kuwaenzi Masheikh waliotumikia dini na kuchangia kukuza malezi na maadili katika jamii kwa kuwasaidia watu wenye uhitaji katika jamii.

Hafla hiyo iliambatana na dua maalum ya kuwaombea Masheikh pamoja na wazazi na ndugu waliotangulia mbele ya haki, huku washiriki wakiiombea Buguruni, Jiji la Dar es Salaam na Taifa la Tanzania liendelee kudumisha amani, mshikamano na maadili mema katika jamii.