Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WANANCHI WAASWA KUEPUKA KUKOPA KWENYE VIKUNDI VISIVYO RASMI

07 Jun, 2024
WANANCHI WAASWA KUEPUKA KUKOPA KWENYE VIKUNDI VISIVYO RASMI

Wajasiriamali kutoka kijiji cha Kaengesa Wilaya ya Sumbawanga vijijini, wakisikiliza semina ya elimu ya fedha kutoka kwa mtaalamu wa Wizara ya Fedha Bw. Jackson Mushumba.  

 

Serikali imetoa rai kwa wananchi kuepuka kukopa fedha kwenye vikundi vinavyotoa huduma za kifedha bila kusajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka athari zinazoambatana na mikopo umiza.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Msimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mshumba, wakati wa semina ya masuala ya fedha iliyofanyika katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

“Tumekuja kubaini kwamba wananchi wengi wako katika vikundi ambavyo havijasajiliwa rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, kwa hiyo nitoe rai kwa wananchi ni vyema wakawa na mwamko wa kujiunga katika vikundi ambavyo ni rasmi na vimesajiliwa kwa mujibu wa Sheria hiyo.”Alisema Bw. Mshumba.

Bw. Mshumba alisema kuwa Serikali inaendelea na program hii ya utoaji elimu vijijini hususan kwa Mkoa wa Rukwa, ambapo wananchi wamepata elimu namna wanavyoweza kuwa na nidhamu ya kujiwekea akiba lakini pia wamepata uelewa juu ya mikopo umiza ili kuepukana na changamoto hii kwa sasa ya mikopo kausha damu.

Alisema kuwa katika mwendelezo wa zoezi hilo imebainika kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa masuala ya mikopo, taratibu za mikopo hawazifahamu lakini pia wananchi wengi hawafahamu masharti yaliyoko katika mikopo wanayochukua kwa watoa huduma mbalimbali.

Bw. Mshumba aliongeza kwa kuwasisitiza wananchi kuwa kabla ya kuchukua mikopo ni vyema wakajiridhisha kuhusu suala la riba, kama mtoa huduma amesajiliwa kwa mujibu wa sheria na pia waelewe vigezo na masharti yaliyopo kwenye mkataba husika.

Alitoa rai kwa wananchi kwa kuwaomba endapo watabaini kwamba kuna vikundi vidogo vya huduma ndogo ya fedha vipo mitaani na havijasajiliwa watoe taarifa kwa mamlaka husika ambazo ni pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye mamlaka zao za Wilaya na Mikoa.

Awali, akizungumza katika semina hiyo Mkazi wa Kijiji cha Kaengesa, Wilaya ya Sumbawanga vijijini, Bi. Rehema Lukali, alisema kuwa ujio wa Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha umewafungua macho kuhusiana na akiba, kwamba ili uaminike katika vyombo vya kifedha lazima mtu awe mwanachama na chama chake kiwe kimesajiliwa kisheria.

Aidha, Bw. Mishek Kassian ambaye pia ni mwana kikundi kikundi cha Kambarage kilichopo katika kijiji cha Lyapona, Wilaya ya Sumbawanga, alisema kuwa kupitia elimu aliyoipata amejifunza mengi na ataenda kuwaelimisha watu wengine maana anaona mikopo mingi inakopeshwa na watu binafsi na taasisi mbalimbali ambapo wengi wanakopa bila kuwa na malengo.

Mwisho