Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WAHITIMU TIA WAHIMIZWA KUTUMIA ELIMU KUBUNI FURSA ZA KIUCHUMI

28 Nov, 2026
WAHITIMU TIA WAHIMIZWA KUTUMIA ELIMU KUBUNI FURSA ZA KIUCHUMI

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akimkabidhi zawadi na cheti mwanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), aliyefanya vizuri katika masomo, Bi. Mwajuma Shija, katika Mahafali ya 24 ya taasisi hiyo, yaliyofanyika katika viwanja vya TIA, jijini Mwanza.

Wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wameagizwa kutumia elimu, ujuzi na teknolojia waliopata kubuni fursa za kiuchumi, kuanzisha biashara na kuzalisha ajira kwa wengine, badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa pekee.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) katika Mahafali ya 24 ya TIA, Kampasi ya Mwanza, ambapo jumla ya wahitimu 1,402 wametunukiwa vyeti na shahada katika fani mbalimbali, wakiwemo wahitimu wa kwanza wa Shahada ya Ualimu katika Uhasibu na Biashara, katika viwanja vya TIA, jijini Mwanza.

Mhe. Luswetula alisema kuhitimu ni hatua ya kuingia katika ulimwengu wa kazi, biashara na uongozi, hivyo wanapaswa kutumia maarifa waliyopata kutengeneza fursa badala ya kusubiri ajira zitoke.

“Msiogope ndoto zenu, thubutuni kuzifanya, hata kama mnaanzia na simu moja tu. Msisubiri kuajiriwa pekee, anzisheni biashara na kuzalisha ajira kwa wengine,” alisisitiza Mhe. Luswetula.

Alisema vijana wanaweza kuanza biashara hata bila kuwa na maduka au ofisi, kwa kutumia simu za mkononi na mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa, kupokea mahitaji ya wateja na kufanya mauzo, hivyo ni muhimu wahitimu kutumia maarifa ya uhasibu na biashara waliyoyapata TIA kuongeza ubunifu, ufanisi na ushindani katika shughuli hizo.

“Mnawajua wale mawinga, hawana duka, hawana ofisi, wanatuma bidhaa mtandaoni, wateja wanaagiza, wanauza. Sasa fikirieni mkiwa na maarifa mliyopata TIA, mnaweza kuongeza ubunifu zaidi,” alifafanua Mhe. Luswetula.

Aliongeza kuwa wahitimu hao wanapaswa kutumia zaidi teknolojia katika kutafuta fursa za biashara, kazi na kutengeneza mifumo bunifu, huku akiwahimiza kuwa waadilifu, kuweka akiba na kuwekeza sehemu ya mapato yao badala ya kutumia fedha zote wanazopata.

“Jina na uaminifu wa mtu ni mtaji muhimu katika kujenga mafanikio ya muda mrefu, hakikisheni shughuli zenu zinafanyika kwa uwazi na uadilifu, mkianzisha biashara, jisajilini, lipeni kodi kwa hiari na mdai risiti halali kwani kodi ndiyo inayojenga madaraja, shule na hospitali, na ndiyo iliyowasomesha ninyi”, aliwasihi Mhe. Luswetula.

 

Aidha, aliwakumbusha wahitimu waliopata mikopo ya elimu ya juu kuwa waadilifu na kutimiza wajibu wa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwawezesha wanafunzi wengine kupata fursa ya kuendelea na masomo.

Pamoja na hayo, aliipongeza TIA kwa kutekeleza Mpango wa Ukuzaji wa Wanafunzi Kitaaluma ambao tangu mwaka 2022 umewezesha takribani wanafunzi 2,500 kunufaika, sambamba na kuandaa mashindano ya mawazo bunifu ya biashara, ambapo mshindi wa kwanza hupata fursa ya kutembelea China au Urusi kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu zaidi.

Alisema jitihada hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kukuza uchumi, hivyo kuitaka Menejimenti ya TIA kuendelea kuunga mkono mawazo bunifu ya wanafunzi ili yakue na kuwa biashara endelevu zinazozalisha ajira na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Mhe. Luswetula alisema Serikali imeendela kutekeleza mikakati ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa Daraja la J.P. Magufuli (kigongo - busisi), lililojengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 611, ambalo limerahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, Meli ya MV New Mwanza, iliyogharimu takribani shilingi bilioni 120, inabeba abiria 1,200, magari 20 na tani 400 za mizigo pamoja na Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Mwanza–Isaka, chenye urefu wa kilomita 341, imefikia zaidi ya asilimia 68.

Alibainisha kuwa uwekezaji huo unaimarisha nafasi ya Mwanza kama kitovu cha biashara na kiunganishi cha Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kufungua fursa katika uvuvi, kilimo, madini, utalii, biashara na huduma za fedha.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Pallangyo, alisema Kampasi hiyo imeendelea kupata mafanikio katika nyanja mbalimbali ikiwemo kufanya na kuchapisha tafiti 22 katika majarida ya kimataifa katika mwaka wa masomo 2025/2026.

Alisema tafiti hizo zimejikita katika maeneo mbalimbali yakiwemo utawala bora, matumizi ya akili unde (AI) katika biashara, mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji na masoko ya hisa, hatua inayolenga kuongeza mchango wa taasisi hiyo katika uzalishaji wa maarifa na kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.

Prof. Pallangyo alisema kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Serikali imetoa takribani Sh. bilioni 7.25 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 336 katika Kampasi ya Mwanza, hatua inayoboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza uwezo wa taasisi kutoa huduma za elimu ya juu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha, Prof. Johaveness Aikaeli, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya Taasisi ya TIA kwa kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa kila wakati.

Alisema Bodi ya Ushauri itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kutoa ushauri wa kimkakati kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ili maendeleo ya TIA yaendane na sera, vipaumbele na mahitaji ya Taifa, huku ikisisitiza ubora wa elimu, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali.

Mwisho.