Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

UTUNZAJI KUMBUKUMBU KURAHISISHA MALIPO YA BIMA

31 Jan, 2024
UTUNZAJI KUMBUKUMBU KURAHISISHA MALIPO YA BIMA

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kusini, Mhe. Dkt. Oscar Kikoyo, kuhusu Sheria ya Bima na swali la Mbunge wa Konde, Mhe. Mohamed Said Issa kuhusu mkakati wa Serikali wa kuongeza mapato ya biashara zinazofanyika kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, bungeni Jijini Dodoma.

 

Serikali imewataka wananchi kutunza kumbukumbu na nyaraka muhimu za rejea ili kuondoa usumbufu na kurahisisha zoezi la ulipaji fidia hususan kwa wasimamizi wa mirathi kupitia bima walizokata.

Wito huo umetolewa bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kusini, Mhe. Dkt. Oscar Kikoyo, aliyetaka kufahamu wakati ambao Serikali itarekebisha Sheria ya Bima ya Tanzania ili kuweka kima cha chini cha malipo ya fidia kwa waathirika wa ajali za barabarani.

Alisema kuwa Septemba 2022, Mamlaka ya Bima Tanzania ilitoa Mwongozo unaotambulika kama Mwongozo wa Viwango Elekezi vya Fidia ya Bima kwa Madai ya Majeraha ya Mwili na Vifo kwa Mtu wa Tatu Kutokana na Ajali za Vyombo vya Moto.

“Mwongozo huo wa Viwango vya Fidia ya Bima ulitolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 6 na 11 cha Sheria ya Bima Sura Na. 394, lengo likiwa ni kuweka usawa na ubora katika ulipaji fidia zitokanazo na madai ya bima”, alisema Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa utekelezaji wa mwongozo huo umepunguza kwa sehemu kubwa malalamiko kutoka kwa waathirika wa ajali za vyombo vya moto kwa kuwa kuna usawa katika suala la viwango vya fidia vinavyotolewa na kampuni za bima.

Aidha alieleza kuwa Serikali itaendelea na jitihada za kujenga uelewa kwa wadau wa tasnia ya bima na wananchi kwa ujumla ili kutimiza matakwa ya Sheria ya Bima, Sura 394, ikiwemo kuboresha huduma za bima na kumlinda mteja.

Kwa upande mwingine, akijibu swali la Mbunge wa Konde, Mhe. Mohamed Said Issa kuhusu mkakati wa Serikali wa kuongeza mapato ya biashara zinazofanyika kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali za pande mbili zimeendelea kuboresha na kutekeleza mikakati mbalimbali kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za uwekezaji na biashara.

Alieleza kuwa baadhi ya mikakati iliyotekelezwa ni pamoja na kuboresha na kuunganisha mifumo ya kodi ya EFDMS na VFMS ili kusomana na kurahisisha utozaji kodi, ada na tozo, kuboresha mifumo ya urejeshaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kurahisisha mifumo ya utoaji vibali, leseni na ukaguzi wa mizigo.

Aidha Mhe. Dkt. Nchemba alibainisha kuwa katika kuongeza uwazi, Serikali kupitia Mamlaka za Usimamizi wa Mapato zimeweka bango linaloonesha bidhaa ambazo hazipaswi kulipiwa ushuru au kodi na bidhaa zinazopaswa kulipiwa, pamoja na viwango vinavyopaswa kulipwa.

Alisema kuwa pande zote zimekubaliana kuwa ushuru wa forodha unaokusanywa kwa upande wa Zanzibar, uwasilishwe kwenye mfumo wa Hazina waSerikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato na ufanisi katika udhibiti wa biashara za magendo

Mwisho.