Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TANZANIA, USWISI NA IRELAND ZASAINI MKATABA WA KUNUSURU KAYA MASIKINI

29 Sep, 2023
TANZANIA, USWISI NA IRELAND ZASAINI MKATABA WA KUNUSURU KAYA MASIKINI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia) na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Didier Chassot (kushoto), wakionesha hati ya makubaliano ya msaada wa Dola za Marekani milioni 18 (sawa na shilingi bilioni 44.4 za Tanzania), kwa ajili ya kufadhili mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili (PSSN II) unaosimamiwa na TASAF, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.

 

Serikali ya Tanzania imesaini mikataba miwili ya msaada yenye thamani ya dola za Marekani milioni 20.3 sawa na shilingi bilioni 50.13 kwa ajili ya kunusuru kaya masikini awamu ya pili (PSSN II).
 
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba alisema msaada huo umetolewa na Serikali ya Uswisi dola za Marekani milioni 18 na Euro milioni 2.2 sawa na dola za Marekani milioni 2.3 zimetolewa na Serikali ya Ireland.
 
"Kiasi cha misaada kilichosainiwa leo ni mwendelezo wa misaada mingine iliyopokelewa kutoka kwa serikali hizi mbili ambapo misaada ya kipindi cha nyuma kwa mpango huu wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili ilikuwa faranga za Uswisi milioni 15.72 sawa na dola za Marekani milioni 17.1 kutoka serikali ya Uswiss na Euro milioni 2 sawa na dola za Marekani milioni 2.1 kutoka serikali ya Ireland. ," alisema Dkt. Mwamba.
 
Alisema misaada hiyo imewezesha serikali kufanya kazi yao kuwa rahisi katika kuleta maendeleo kwa watanzania wote.
 
Aidha, PSSN II inaendana na Dira ya Tanzania ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo inatoa mwelekeo wa juhudi za kuleta maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii hadi kufikia mwaka 2025.
 
"Dira hii kwa sasa inatekelezwa kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2025/26 ," alisema Dkt. Mwamba.
 
Alisema kwamba pia misaada hii pia inaendana na lengo la kwanza la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambalo linalenga kuondoa umaskini wa aina zote ifikapo mwaka 2030, na ajenda ya Afrika ya mwaka 2063 ambayo inalenga kuwezesha mpango wa Afrika kufikia ukuaji jumuishi na endelevu wa uchumi na maendeleo ifikapo mwaka 2063.
 
Alisema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umewezesha wanafunzi kutoka Kaya maskini kupata elimu ya sekondari na elimu ya Juu. Mwaka 2022 wanafunzi 2,950 kutoka kaya maskini walipata mkopo wa asilimia 100 kutoka bodi ya mikopo ya Elimu ya juu chini ya msaada wa PSSN II.
 
Aidha alisema ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeanza kuimarika ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2023 ukuaji ulikuwa ni asilimia 5.6.
 
Alisema kwa mwaka 2019 kabla ya UVIKO – 19, uchumi wa Tanzania ulikuwa unakuwa kwa asilimia 7 lakini ukuaji huo ulishuka na kuwa asilimia 4.8 mwaka 2020 kutokana na madhara ya UVIKO – 19 na mwaka 2021 ukuaji ulipanda hadi asilimia 4.9 kabla ya kushuka kuwa asilimia 4.7 mwaka 2022 kutokana na madhara ya vita vya Ukraine na Urusi.
 
"Natumaini misaada yenu kupitia PSSN II itawezesha kaya nyingi maskini kuondokana na umaskini na kuchangia ukuaji wa pato la taifa," alisema Dkt. Mwamba.
 
Dkt. Mwamba alisema bajeti yote ya PSSN II ni dola za Marekani milioni 883.32 ambapo watafikia malengo yaliyokusudiwa ifikapo mwishoni mwa PSSN II mwwezi Septemba 2025 kwa kuwezesha kaya maskini kupata huduma za kijamii na kiuchumi.
 
 
Dkt. Mwamba alisema Serikali za Uswisi na Ireland siyo tu wanachangia kwa mpango wa kunusuru kaya maskini lakini pia wanachangia sekta nyingine zikihusisha Afya, Elimu, Haki za Binadamu, Utawala bora na Demokrasia.
 
Dkt. Mwamba aliwahakikishia utayari wa Serikali chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kuimarisha ushirikiano na nchi hizo kwa maendeleo ya watu wetu na kuahidi kuwa msaada uliotolewa utatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray, alisema PSSN II itaboresha upatikanaji wa fursa za mapato na huduma za kijamii na kiuchumi kwa kaya zenye uhitaji sambamba na kuimarisha na kulinda rasilimali watu ya watoto wao.
 
Alisema TASAF hadi sasa imefikia walengwa milioni Moja na laki tatu huku wakiwa wametoa ruzuku ya shilingi bilioni 7.78, pia wametoa ajira 760,000 na vikundi 50,000 vimewezeshwa kiuchumi.
 
"PSSN II itafikia malengo yake kupitia utekelezaji wa hatua zilizojumuishwa, kuongeza mapato ya kaya kupitia kujenga na kufanya kaya kujiamini, kuimarisha udhibiti na kuwezesha kuwepo kwa ajira zenye tija zaidi," alisema Mziray .
 
Naye Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Didier Chassot, alisema msaada walioutoa ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Uswisi, tangu mwaka 2020 serikali ya Uswisi imekuwa itoa misaada kwenye PSSN .
 
Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Mary O'neil, alisema ushirikiano wa Tanzania na Ireland ni wa zaidi ya miaka 40, kwa kipindi hicho chote wamekuwa wakisaidia katika kuwawezesha wanawake, sera, amani na kaya masikini.
 
Mwisho