Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TANZANIA NA KENYA ZAAZIMIA KUIMARISHA ZAIDI UHUSIANO WA KIUCHUMI, KIBIASHARA NA KIDIPLOMASIA.

08 Oct, 2026
TANZANIA NA KENYA ZAAZIMIA KUIMARISHA ZAIDI UHUSIANO WA KIUCHUMI, KIBIASHARA NA KIDIPLOMASIA.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (katikati), Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Kirumba Karemu (wa tatu kushoto), Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, anayesimamia Masuala ya Usimamizi wa Fedha, Bi. Asha Khamis Abdulla (wa tatu kulia), Mkurugenzi wa Mfumo wa Taarifa za Fedha na Huduma za Teknolojia ya Habari (TEHAMA), Dkt. John Sausi (wa pili kulia) na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje Bw. James Msina (wa kwanza kulia), wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao kilichojadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Kenya. Mazungumzo hayo yamejikita katika kuangalia fursa za kuimarisha mahusiano na ushirikiano katika sekta ya fedha na maeneo mengine yenye maslahi ya pamoja, ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na kuendeleza utekelezaji wa mipango ya pamoja kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Kenya zimeazimia kuendelea kushirikiana katika kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs) vinavyoathiri mtiririko wa bidhaa, huduma na mitaji baina ya nchi hizo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha biashara na ushirikiano wa kiuchumi.

Kauli hiyo ilitolewa tarehe 7 Oktoba, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, wakati akizungumza na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Kirumba Karemu, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Lengo kuu la ziara ya Balozi Karemu lilikuwa ni kujitambulisha rasmi katika Wizara ya Fedha, ambayo ni mdau wa kimkakati katika kusimamia na kuendesha masuala ya mtangamano wa kifedha ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Itakumbukwa kuwa Balozi Karemu aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto mnamo mwaka 2026, kuwa Balozi Mkaazi wa Kenya nchini Tanzania.

Dkt. Mwamba alisema Wizara ya Fedha, kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, inaendelea kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto, kuhusu kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi na kurahisisha mtiririko wa bidhaa, huduma na mitaji kati ya nchi hizo.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya, ambao umejengwa katika misingi ya maslahi ya pamoja, diplomasia ya kiuchumi na ushirikiano wa kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Aidha, Dkt. Mwamba alisema, katika kipindi cha mwaka 2026, Tanzania na Kenya zimeendelea kufanya mazungumzo na kuchukua hatua mbalimbali za kushughulikia zaidi ya vikwazo 50 visivyo vya kikodi vilivyokuwa vikiathiri biashara kati ya nchi hizo.

Amesema katika Mkutano wa 10 wa Kamati ya Pamoja ya Biashara (JTC) kati ya Tanzania na Kenya uliofanyika Mombasa, Kenya, Aprili 13 hadi 17, 2026, pande hizo zilipendekeza na kukubaliana kuondoa vikwazo hivyo na kurahisisha biashara ya bidhaa na huduma.

Dkt. Mwamba pia alieleza kuwa, katika mazungumzo ya pande mbili yaliyofanyika mwezi Mei 2026, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. William Ruto walishuhudia utiaji saini wa Mikataba na Hati za Makubaliano (MoUs) nane (8) katika  maeneo mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo maendeleo ya reli, usafirishaji wa baharini kupitia Bandari za Dar es Salaam na Mombasa, kilimo na nishati, ikiwemo pendekezo la ujenzi wa bomba la gesi asilia.

Aidha, amesema viongozi wa nchi wanachama wa EAC, kupitia Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo uliofanyika Machi 2026, walielekeza nchi wanachama kushughulikia na kuondoa vikwazo vyote visivyo vya kikodi katika biashara ifikapo Juni 30, 2026.

“Hili ni eneo ambalo napendekeza tuendelee kushirikiana katika kipindi chako cha utumishi hapa Tanzania,” alisema Dkt. Mwamba.

Dkt. Mwamba alisema suala la kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi linatarajiwa pia kuendelea kujadiliwa katika kikao kijacho cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Tanzania na Kenya (JCC), kinachotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 12 hadi 14, 2026.

Alifafanua kuwa kikao hicho kitatoa fursa kwa pande hizo kuendelea kujadili changamoto zilizopo na kutafuta ufumbuzi wa masuala yanayohusu ushirikiano wa Tanzania na Kenya.

Dkt. Mwamba amemhakikishia Balozi Karemu kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na Serikali ya Kenya kupitia taasisi husika katika kushughulikia changamoto zinazoweza kuathiri biashara na ushirikiano wa kiuchumi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza mahusiano ya muda mrefu kati ya Tanzania na Kenya.


Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Kirumba Karemu, alisema Kenya na Tanzania zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala ya fedha na biashara, ikiwemo kurahisisha huduma za malipo ya mipakani, kuoanisha mifumo ya kodi na kuboresha huduma katika vituo vya pamoja vya mipakani.

Balozi Karemu alipongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) ambao unachagiza biashara kati ya nchi hizi mbili.

Alisema juhudi hizo zinapaswa kwenda sambamba na kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi, kuoanisha takwimu za biashara na kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi, hatua zitakazochangia kuimarisha zaidi mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Balozi Karemu amemshukuru Dkt. Mwamba kwa kumpokea na kueleza dhamira yake ya kuendelea kuchangia katika kuimarisha mahusiano ya Tanzania na Kenya, ikiwemo ushirikiano wa kikanda na uwezeshaji wa diaspora.

Mwisho