Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TANZANIA NA DENMARK KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

09 Mar, 2023
TANZANIA NA DENMARK KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiagana na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jorgesen, baada ya kumaliza mazungumzo yaliyofanyika Doha nchini Qatar.

 

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa Dermark imekubali kushirikiana na Tanzania katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekua yakiathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Dkt. Nchemba ameyasema hayo mjini Doha nchini Qatar, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Kifalme ya Denmark, Mhe. Dan Jorgesen, kando ya Mkutano wa Tano wa Umoja wa  Mataifa wa nchi zinazoendelea za kipato cha chini unaoendelea nchini humo.

Alisema nchi hizo mbili zimekubaliana kuzielekeza Taasisi zao kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali hususani kukabiliana na mabadiliko hayo ya tabia nchi ili kukuza uchumi.

“Licha ya makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huu, tumekua na ushirikiano mzuri na Dernmark ambapo Serikali yetu hupokea fedha nyingi kupitia Taasisi za Denmark ambazo hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo”, alisema Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa mkutano kati ya nchi hizo mbili ni mwendelezo wa mikutano mbalimbali ambayo imekuwa ikifanyika hivyo mazungumzo ya sasa ni jitihada za kuendelea kuimarisha ushirikiano huo wa kimaendeleo katika sekta mbalimbali.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt.  Saada Mkuya Salum, alisema kuwa Serikali ya Zanzibar imepata manufaa makubwa katika sekta za kijamii ikiwemo  afya, elimu na miundombinu.

Alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha inatekeleza diplomasia ya kiuchumi na nchi mbalimbali ili kuvutia uwekezaji na kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo mikutano inayoendelea na nchi nyingine ni miongoni mwa jitihada za kufanikisha azma hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jorgesen, ameipongeza Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo.

Mhe.  Jorgesen amesema kuwa pamoja na upya wa Serikali yake iliyopo madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa Novemba 2022, Serikali ya mseto ya Denmark itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

“Mabadiliko ya Tabianchi ni masuala ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele na kila mmoja wetu kutokana na athari zinazoendelea kujitokeza kutokana na changamoto hiyo”, alisema Mhe. Jorgesen.

Aidha, Mhe.  Jorgesen alisema Serikali yake inayoongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Mette Frederiksen, anao ufahamu mkubwa kuhusu siasa za Bara la Afrika hivyo itasaidia kuongeza ushirikiano kati ya Denmark na Tanzania.