Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAWAZIRI WA AFRICA - FEDHA NA JINSIA

14 Nov, 2023
TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAWAZIRI WA AFRICA - FEDHA NA JINSIA
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (wapili kulia), Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima (Mb) (wapili kushoto), Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women), Bi. Hodan Addou (kushoto) na Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF Afritac East), Bi. Xiangming LI (kulia), wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano na wanahabari kuhusu Mkutano wa Mawaziri wa Afrika wanaohusika na Masuala ya Fedha na Jinsia kutoka nchi 22 wanachama wa Jukwaa la Usawa wa Kijinsia (UN Women) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF Afritac East), utakaofanyika jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotana, kuanzia tarehe 15 hadi 17, Novemba, 2023. Mkutano huo unaolenga kujadili kuhusu ufadhili wa usawa wa kijinsia unatarajiwa ushiriki kutoka Nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Burundi, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, Eritrea, Ethiopia, Guinea, Ivory coast, Nigeria, Senegal, Kenya, Liberia, Madagascar, Malawi, Msumbiji, Somalia, Afrika Kusini, Rwanda, Sudan ya Kusini, Zambia, Zimbabwe na Uganda.
 
 
 
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Afrika wanaohusika na Masuala ya Fedha na Jinsia kutoka nchi 22 wanachama wa Jukwaa la Usawa wa Kijinsia (UN Women) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF-Afritac East), utakaofanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 15 hadi 17, Novemba, 2023.
 
Wakizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima, wameeleza kuwa Mkutano huo unalenga kujadili kuhusu namna yakuwawezesha wanawake na wasichana kiuchumi na kijamii kupitia ufadhili wa usawa wa kijinsia.
 
Nchi zinazotarajiwa kushiriki Mkutano huo ni Tanzania, Burundi, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, Eritrea, Ethiopia, Guinea, Ivory coast, Nigeria, Senegal, Kenya, Liberia, Madagascar, Malawi, Msumbiji, Somalia, Afrika Kusini, Rwanda, Sudan ya Kusini, Zambia, Zimbabwe na Uganda.
 
Walisema kuwa Mawaziri hao watajadili namna bora ya kushughulikia athari za mapungufu ya kijinsia katika uchumi-jumla na kuchochea ufadhili wa masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).
 
“Mkutano wa Mawaziri utaangazia hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa ahadi zilizowekwa na Jukwaa la Usawa wa Kijinsia, athari za uchumi jumla katika usawa wa kijinsia na jukumu la upangaji bajeti unaozingatia jinsia” Alisema Dkt. Nchemba.
 
Walisema kuwa matokeo yanayotegemewa kwenye mkutano huo wa ngazi ya juu wa Mawaziri ni uwepo wa vipaumbele vya kuharakisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na ahadi ya kugharamia utekelezaji kutoka kwa washiriki wa Mkutano huo.
 
Naye, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima, amesema kuwa ujio wa Mkutano huo unaakisi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo inataka mipango ya nchi iendane na mizania ya usawa wa kijinsia.
 
Kwa upande wao, Mkurugenzi wa IMF Afritac East, Bi. Xiangming LI na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja la Wanawake (UN-Women), Bi. Hodan Addou, wameeleza kuwa mchango wa wanawake katika uchumi na maendeleo ya kijamii barani Afrika umekuwa mdogo ikilinganishwa na wanaume.
 
Walisema kuwa asilimia 47 tu ya wanawake wanashiriki katika sekta zinazojenga uchumi mpana kupitia soko la ajira ikilinganishwa na asilimia 72 ya wanaume na kwamba kuna kila sababu ya kuboresha hali hiyo.
 
Mkurugenzi wa IMF Afritac, Bi. LI aliema kuwa matarajio ya Jukwaa hilo ni kuona pengo hilo likipunguzwa hata kwa asilimia 6 tu, mchango wa wanawake katika uchumi wa nchi za Afrika utafikia asilimia 8 ya pato la Taifa la nchi wanachama.
 
Bi. LI, alizishukuru nchi zinazochangia mpango huo ambazo ni China, Umoja wa Ulaya, Ujerumani, The Netherlands, Norway, Switzerland na Uingereza, ambazo mchango wao pia umewezesha mkutano huo kufanyika nchini Tanzania.
 
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na masuala ya Usawa wa Kijinsia (UN-Women), Bi. Hodan Addou, aliipongeza Tanzania kwa kuwa kinara katika masuala ya kusaidia maendeleo ya jamii hususani wanawake na Watoto kupata haki zao za kiuchumi na kuwezesha mkutano huo kufanyika nchini Tanzania.
 
Alisema kuwa Shirika lake, kwa kushirikiana na nchi wanachama, litaongeza ufadhili katika masuala ya usawa wa kijinsia ili kuwawezesha wanawake na wasichana kutoka nchi wanachama kwa kuwaunganisha na wafadhili ili kuharakisha maendeleo ya kundi hilo.
 
Mwisho