Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA HISPANIA KUKUZA UCHUMI

28 Apr, 2026
TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA HISPANIA KUKUZA UCHUMI

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa pili kulia) na Balozi wa Hispania nchini Tanzania Mhe. Paloma Serra Robles wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa kwanza kulia) na Kushoto ni Mshauri wa masuala ya uchumi na biashara-ubalozi wa Hispania nchini Tanzania, Bi. Rocio Kessler Grijalvo, baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.

 

Serikali imeeleza kuwa iko tayari kushirikiana na Hispania katika maeneo ya kipaumbele ikiwemo kukuza uchumi endelevu, ujenzi wa miundombinu, mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na kuendeleza rasilimali watu, kwa lengo la kuchochea maendeleo jumuishi nchini.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Hispania chini, Mhe. Paloma Serra Robles, aliyefika kwa ajili kujitambulisha na kuwasilisha masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Hispania, katika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, Dodoma.

Mhe. Balozi Omar alisema dhamira ya Serikali ni kuendelea kushirikiana na Hispania katika kutafuta rasilimali za kifedha kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo yenye maslahi mapana kwa Taifa, lengo likiwa ni kuchochea ukuaji wa uchumi na huduma bora kwa jamii.

‘‘Uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Hispania ni wa muda mrefu, ambapo kampuni za Hispania zimekuwa zikiwekeza nchini katika sekta mbalimbali, ikiwemo utalii, pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo na zitaendelea kuja kuwekeza nchini kwa kuwa mwelekeo wa Serikali ya Hispania ni kuongeza ushirikiano wa pamoja wenye mandeleo endelevu ikiwemo kuunganisha kampuni za Tanzania na kampuni za Hispania’’, alisema Mhe. Balozi Omar.

Pia Mhe. Omar alitoa wito kwa kampuni na wawekezaji kutoka Hispania kuja kuwekeza nchini Tanzania na kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kutoa vivutio mbalimbali vya kikodi na uwekezaji vinavyoendana na ukubwa wa miradi, ikilenga kukuza ushirikiano.

Aliishukuru Hispania kwa kufadhili utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini, ikiwemo kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 30 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Msimbazi, jijini Dar es Salaam ambao unatarajiwa kuleta mabadiliko katika kukabiliana na changamoto za mafuriko, kuimarisha hifadhi ya mazingira, na kukuza ustahimilivu wa miundombinu ya jiji hilo dhidi ya majanga ya asili.

Akizungumza kuhusu uchumi wa Tanzania Mhe. Omar alisema kuwa uchumi umeendelea kuimarika kwa kasi baada ya Pato la Taifa (GDP) kukua hadi kufikia asilimia 6.4 katika robo ya tatu ya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 6.1 katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Aliongeza kuwa mfumuko wa bei umesalia kuwa tulivu kwa wastani wa asilimia 3.5 hadi kufikia Desemba 2025, ndani ya malengo ya kitaifa ya kati ya asilimia 3 na 5, huku kikiwa chini ya viwango vya ukomo vilivyowekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Utulivu huo wa bei za bidhaa na huduma unatajwa kuwa kigezo muhimu kinachojenga imani kwa wawekezaji na kutoa fursa pana kwa washirika wa maendeleo kuendelea kuwekeza nchini kutokana na mazingira tabiri ya uchumi mkuu.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuimarisha ushirikiano wa pande hizo mbili kwa ajili ya maendeleo na ustawi wananchi na kumpongeza kwa kuteuliwa kwake kuwa Balozi wa nchi hiyo.

Kwa upande wake Balozi wa Hispania nchini, Mhe. Paloma Serra Robles, ameeleza dhamira ya nchi yake kuendelea kuisaidia Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta tofauti zikiwemo miundombinu ya usafirishaji na miradi ya kijamii yenye tija kwa wananchi.

Alisema nchi hiyo imesaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo wa uendelezaji wa bonde la msimbazi ambao kukamilika kwake kutaleta tija kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El -maamry Mwamba, Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Madeni,  Bw. Omary Khama, Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Bw. James Msina pamoja na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano Wa Afrika Mashariki.

MWISHO.