Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TAARIFA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHE. DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA

12 Nov, 2021
TAARIFA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHE. DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), KWA  VYOMBO VYA HABARI  KUHUSU MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU  WA TANZANIA BARA

UTANGULIZI

Ndugu Wanahabari, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetuwezesha kukutana hapa leo tukiwa na afya njema. Pia napenda kuchukua fursa hii tena kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake kwa nchi hii ambayo ameijalia tunu za amani, utulivu, mshikamano, umoja na mtangamano katika kipindi chote cha miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu. Tunu hizo zimetuwezesha kuendelea na shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa na pia kutoa fursa kwa wananchi kuweza kufanyia shughuli zao za maendeleo.

 

Ndugu Wanahabari, Wizara ya Fedha na Mipango inatambua mchango wenu katika kuwaelimisha na kuwafikishia wananchi taarifa muhimu zinazohusu masuala ya kiuchumi na kijamii ili umma wa Watanzania uweze kuhabarishwa. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana kwa mchango wenu huu mkubwa kwa Taifa.

 

Ndugu Wanahabari, kama tunavyofahamu sasa hivi tuko katika kipindi cha maandalizi ya kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru tulioupata kutoka kwa mkoloni mwaka 1961. Sote tunafahamu kuwa tangu wakati huo, jitihada mbalimbali zilifanyika zikiongozwa na viongozi wakuu wa nchi yetu nchini ya utawala wa chama cha TANU na baadae CCM kuanzia mwaka 1977. Ni kipindi ambacho uchumi wa nchi yetu umeendelea kuwa imara japo ulipitia katika vipindi mbalimbali vya mabonde na milima.

 

MWENENDO WA UKUAJI WA UCHUMI

 

Ndugu Wanahabari, Tangu uhuru, uchumi wa Tanzania umepitia katika nyakati mbalimbali za mafanikio ya kiuchumi pamoja na changamoto kadhaa zikiwemo ukame katika miaka ya mwanzoni mwa 1970 na 2012, mdororo wa uchumi wa mwaka 2008, vita vya Kagera mwaka 1978 pamoja na ugonjwa wa UVIKO mwaka 2020. Hata hivyo, Serikali kupitia mikakati mbalimbali iliweza kujikwamua kutokana na magumu hayo iliyopitia na hii iliwezesha katika historia ya Tanzania kutokuwa na ukuaji hasi wa uchumi (recession) tangu uhuru. Takwimu zinaonesha kuwa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka sitini ya uhuru ulikuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali lakini haujawahi kufikia ukuaji hasi. Wastani wa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha Serikali ya awamu ya kwanza (1967 – 1985) iliyoongozwa na mwasisi na Baba wa Taifa hili Hayati Mwalim Juluis Kambarage Nyerere ulikuwa asilimia 3.1; Serikali ya awamu ya pili (1986 – 1995) asilimia 3.0, Serikali ya awamu ya tatu (1996 – 2005) asilimia 5.7, Serikali ya awamu ya nne (2006 – 2015) asilimia 6.3, na Serikali ya awamu ya tano (2016 – 2020) asilimia 6.5.

 

Ndugu Wanahabari, mwaka 2020, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019. Sababu kuu ya kupungua kwa kasi ya ukuaji ni athari za hatua zilizochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani ambao ni washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania katika kukabiliana na janga la UVIKO-19. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na mataifa hayo ni pamoja na kufunga mipaka, kusitisha safari za ndege za kimataifa na kusitisha baadhi ya shughuli za kiuchumi zinazohusisha mikusanyiko. Hatua hizo zilisababisha uchumi wa dunia kuporomoka mwaka 2020 ambapo nchi nyingi zilikuwa na ukuaji hasi na kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni nchi 11 tu zilikuwa na ukuaji chanya kati ya nchi 45. Pamoja na kupungua kwa kasi ya ukuaji, Tanzania iliweza kuwa na ukuaji chanya kutokana na kutochukua hatua za kuzuia kufanyika kwa shughuli za kiuchumi isipokuwa kwa kipindi kifupi tu cha robo ya pili ya mwaka 2020 ambapo ilisitisha kwa muda baadhi ya shughuli zinazohusisha mikusanyiko ya watu kama shule, sanaa na burudani. Athari za janga la UVIKO-19 zilijitokeza zaidi katika shughuli za kiuchumi za malazi na huduma ya chakula pamoja na sanaa na burudani ambazo zilikuwa na ukuaji hasi mwaka 2020.

 

Ndugu Wanahabari, Serikali ya awamu ya sita imeingia madarakani katika kipindi ambacho dunia bado inapambana na athari za kiuchumi na kijamii za janga la UVIKO-19. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021, (Januari – Juni) uchumi umekua kwa asilimia 4.7 ikilinganishwa na asilimia 5.0 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Kupungua kwa kasi ya ukuaji katika kipindi hicho kumetokana na athari za UVIKO-19 katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Shughuli nyingi za kiuchumi zimeendelea kuwa na viwango chanya vya ukuaji katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021 ingawa kasi yake ilipungua ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2020. 

 

TANZANIA KUINGIA KATIKA UCHUMI WA KATI

Ndugu Wanahabari, Tanzania ilikuwa nchi ya kipato cha chini kwa miaka 59 tangu kupata uhuru hadi mwaka 2020 Benki ya Dunia ilipoitangaza kwa mara ya kwanza kuwa nchi ya Uchumi wa Kati wa Chini. Hii ni baada ya mageuzi makubwa ya kiuchumi yaliyofanyika ambayo yalipelekea wastani wa pato kwa mtu (Per capita GNI) kuvuka kiwango kilichowekwa na Benki ya Dunia cha dola za Marekani 1,036 kufikia dola za Marekani 1,100 mwaka 2019. Mwaka 2020, uchumi wa nchi nyingi duniani uliyumba lakini pamoja na kasi ya ukuaji wa Tanzania kupungua bado tulifanikiwa kubaki ndani ya kundi la nchi za kipato cha kati cha chini kwa wastani wa Pato kwa mtu la dola za Marekani 1,080. Tanzania iliingia katika kundi la nchi ya uchumi wa kati mapema zaidi ikilinganishwa na malengo ya Dira ya Taifa ya kufikia hadhi hiyo mwaka 2025. Hii ilitokana na matokeo chanya katika vigezo vya kiuchumi ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, utulivu wa thamani ya shilingi na mfumuko wa bei uliobaki katika wigo wa tarakimu moja kwa muda mrefu. 

 

Ndugu Wanahabari, wastani wa Pato kwa mtu ulikuwa unaongezeka mwaka hadi mwaka kutoka wastani wa dola za Marekani 178.3 (1990 – 1995), wastani wa dola za Marekani 365 katika serikali ya awamu ya tatu, dola za Marekani 747 awamu ya nne, na wasatani dola za Marekani 1,010 awamu ya tano kwa kutumia kipimo cha Atlas cha Benki ya Dunia. Halikadhalika, kiwango cha umaskini kimeendelea kupungua ambapo kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kimepungua hadi asilimia 25.7 mwaka 2020 kutoka asilimia 38.6 mwaka 1992. Kupungua kwa kiwango cha umaskini kumetokana na jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za msingi za jamii ikiwemo upatikanaji wa maji, umeme, huduma za afya, utoaji wa elimumsingi bila ada na uwezeshaji wa kaya maskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF). 

 

MFUMUKO WA BEI

Ndugu Wanahabari, mfumuko wa bei nao ulipitia katika nyakati mbalimbali za kupanda na kushuka. Kiwango cha juu kabisa cha mfumuko wa bei kilikuwa mwaka 1984 (asilimia 36.1), mwaka 1990 (asilimia 35.9) na mwaka 1994 (asilimia 35.3). Sababu kubwa ilikuwa ni kutokana na ukame na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia. Aidha, mara ya mwisho kuwa na mfumuko wa bei wa tarakimu mbili ilikuwa mwaka 2012 ambao ulifikia asilimia 16.1. Baada ya hapo, mfumuko wa bei umeendelea kupungua mfululizo hadi sasa.

 

Ndugu Wanahabari, katika kipindi cha miaka nane (8) mfululizo iliyopita (2013 – 2020), mfumuko wa bei umeendelea kuwa wa tarakimu moja na kubakia ndani ya malengo tuliyojiwekea sambamba na vigezo (convergency criteria) vilivyowekwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (asilimia 8) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (asilimia 3 – 7). Mwaka 2020, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.3 ikilinganishwa na asilimia 3.4 mwaka 2019. Kushuka kwa kiwango cha mfumuko wa bei kulitokana na sababu mbalimbali zikiwemo utekekezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kutengamaa kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, kuimarika kwa thamani ya shilingi dhidi ya sarafu nyingine duniani, na kuimarika kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika masoko ya ndani na nchi jirani.

 

Ndugu wanahabari, Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha bei ya bidhaa na huduma ikiwemo vifaa vya ujenzi kama vile saruji, nondo, bati, marumaru hazipandishwi kiholela. Jitihada hizo ni pamoja na kufanya majadiliano na wazalishaji ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kudhibiti usambaji ili kuendana na mahitaji na hivyo kupunguza uwezekano wa kuongezeka kwa mfumuko wa bei.

 

SEKTA YA FEDHA

Ndugu wanahabari, Sekta ya fedha ni miongoni mwa sekta muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini. Hadi miaka ya 1990 sekta ya fedha ilihusisha sekta ya benki pekee. Kutokana na mahitaji ya huduma za kifedha kuongezeka, sekta ya fedha imekuwa ikifanyiwa maboresho mbalimbali ikiwemo ‘First and second generation financial sector reforms”. Maboresho hayo yaliweka mazingira wezeshi katika sekta ya fedha kwa kutungu sera, sheria, kanununi na miongozo ya uendeshaji wa sekta hiyo. Kupitia maboresho hayo, Serikali ilianzisha sekta ndogo za masoko ya mitaji na dhamana, mifuko ya hifadhi ya jamii, bima na huduma ndogo za fedha. Hadi mwaka 2020, kulikuwa na benki na taasisi za fedha 55, kampuni za bima 32, kampuni za soko na mitaji 28 na mifuko ya hifadhi ya jamii 2. Kwa upande wa sekta ndogo ya fedha hadi Agusti 2021 kulikuwa na watoa huduma ndogo za fedha daraja la pili (Non deposite taking) 549, watoa ndogo za fedha daraja la tatu (SACCOSS) 460 na watoa huduma ndogo daraja la nne (Vikundi vya kijamii vya huduma dogo za fedha) 11,149. Jitihada hizo zimewezesha kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha kutoka asilimia 56 mwaka 2013 hadi asilimia 65 mwaka 2017 na inatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 75 mwaka 2022. Hii inaenda sambamba na mageuzi ya kiteknolojia yaliyowezesha kutumia mitandao ya simu za mkononi kuanzia miaka ya 2000 mwanzoni kufikisha huduma za fedha maeneo mengi nchini yakiwemo yale ambayo hayana matawi ya benki.

 

KIWANGO CHA KUBADILISHA FEDHA

Ndugu Wanahabari, katika kipindi cha mwaka 1966 hadi 1992 Serikali ilikuwa ikidhibiti viwango vya kubadilisha fedha (Fixed exchange rate). Utaratibu huu  kwa kiwango kikubwa ulichangia mdororo wa uchumi katika miaka ya 1980 kwani thamani ya shilingi ilishuka kwa kiwango kikubwa na kusababisha akiba ya fedha za kigeni kupungua na kuongezeka kwa mfumuko wa bei. Katika kipindi hicho, Serikali ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na mdodoro wa uchumi zikiwemo Structural adjustment Program (1982-1983) na Economic recovery program I &II (1986 & 1989). Kufuatia maboresho hayo, Tanzania ilianza kutumia viwango vya ubadilishaji fedha vinavyotegemea bei ya soko (Floating exchange rate policy) mwaka 1993. Utekelezaji madhubuti wa sera hiyo umeendelea kuimarisha thamani ya shilingi dhidi ya dola ya marekani na sarafu nyingine duniani. Tangu mwaka 1993 Serikali ilipoanza kutumia mfumo wa soko huria, thamani ya shilingi kwa sehemu kubwa ilikuwa inapungua japo kwa kiwango kidogo cha tarakimu moja. Hata hivyo, kiwango cha juu kabisa cha kuporomoka kwa thamani ya shilingi tangu wakati huo kilikuwa asilimia 20.1 mwaka 2015 na baada ya kuimarishwa kwa usimamizi katika sekta hiyo, thamani ya shilingi ilikuwa inapungua kwa kasi ndogo ya chini ya asilimia tatu (asilimia 3).

 

MWENENDO WA MAPATO YA NDANI

Ndugu Wanahabari, japo kulikuwa hakuna utaratibu wala mifumo madhubuti ya ukusanyaji wa mapato, katika Serikali ya awamu ya kwanza iliweza kukusanya mapato ya ndani ya jumla ya shilingi milioni 5,557.3 kati ya mwaka 1966 – 1985. Kiasi hicho kilichokusanywa katika kipindi hicho kilikuwa cha wastani wa asilimia 18.3 ya Pato la Taifa. Jitihada mbalimbali ziliendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuimarisha usimamizi wa mapato ikiwemo kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania mwaka 1997 na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Jitihada hizo zilizaa matunda ambapo mapato ya ndani yaliongezeka kufikia wastani wa shilingi milioni 130,853 katika kipindi cha awamu ya pili, wastani wa shilingi milioni 954,339 katika kipindi cha awamu ya tatu, wastani wa shilingi milioni 6,403,888 katika kipindi cha awamu ya nne, na wastani wa shilingi milioni 18,957,084 katika kipindi cha awamu ya tano.

 

Ndugu Wanahabari, pamoja na mapato kuongezeka mwaka hadi mwaka yamekuwa hayafikii malengo tuliyoweka kwa mwaka husika. Hii ni changamoto inayotufanya kushindwa kufikia malengo yetu ya kuwafikishia wananchi huduma za msingi pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mathalani katika mwaka 2020/21 mapato ya ndani yalifikia asilimia 85.6 ya lengo. Mapato ya ndani yaliyokusanywa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2021/22 yalifikia shilingi bilioni 5,492.1 sawa na asilimia 89.0 ya lengo la shilingi bilioni 6,170.9.     Kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato ya ndani kulitokana na sababu mbalimbali ikiwemo baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kodi hususan kupitia njia za magendo, uhamishaji wa faida kwa kampuni zenye mtandao wa kimataifa na kutokutoa stakabadhi za kielektroniki wakati mauzo yanapofanyika hivyo kuathiri ukusanyaji wa mapato na uwepo wa majanga kama vile kama vile UVIKO – 19 ulioathiri shughuli za kiuchumi na kibiashara.

 

MWENENDO WA MATUMIZI YA MAENDELEO

 

Ndugu wanahabari, kabla ya mwaka 2015 bajeti ya Serikali ya maendeleo ilikuwa chini ya asilimia 25 ya bajeti yote. Hata hivyo, mwaka 2015/16 Serikali lifanya maamuzi ya kuhakikisha bajeti ya maendeleo inaongezeka na kufikia kati ya asilimia 30-40 ya bajeti yote. Hatua hii pamoja na mambo mengine iliwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati kwa ajili ya kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) ambapo tangu uhuru Tanzania imekuwa ikitumia reli iliyojengwa na mkoloni kwa kiwango cha mita geji. Kutokana na mabadiliko ya teknolojia na kuongezeka kwa mahitaji, Serikali ilifanya uamuzi wa kutengeneza reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR) itakayounganisha Tanzania na nchi jirani ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam - Morogoro (km 300) umefikia asilimia 93.0. Aidha, tangu nchi ipate uhuru Serikali ilikuwa na wazo la kutekeleza mradi wa kufua umeme katika bwawa la Mto Rufiji ili kuongeza uzalishaji wa umeme kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya majumbani na viwandani pamoja na kupunguza gharama za uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta. Wazo hilo halikutekelezwa hadi mwaka 2016 ndipo Serikali iliamua kuanza utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere utakaozalisha Mw. 2115 ambapo ujenzi umefikia asilimia 55.6. miradi mingine ni pamoja na: usambazaji wa umeme vijijini ambapo vijiji 10312 kati ya 12,317 sawa na asilimia 83.7 vimeunganishwa na huduma ya umeme; ujenzi wa barabara na madaraja ambapo hadi 2021 mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami umefikia km 13,643.45; na uboreshaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na upatikanaji wa maji.

 

NAKISI YA BAJETI

Ndugu wanahabari, katika historia ya nchi hii, tulishawahi kuwa na akiba ya bajeti (budget surplus) kwa miaka mitatu tu tangu uhuru nayo ni mwaka 1989 (shilingi milioni 6,782), mwaka 1990 (shilingi milioni 8,052) na mwaka 1991 (shilingi milioni 9601). Miaka mingine yote kwa takwimu zilizopo toka mwaka 1966 ilikuwa na nakisi ya bajeti (Budget deficit). Uwiano wa nakisi ya bajeti kwa Pato la Taifa ulikuwa mkubwa miaka ya mwishoni mwa 1970 na mwanzo mwa 1980 kwa wastani wa asilimia 7 ya pato la Taifa. Hata hivyo, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi, hali iliyowezesha kurejesha nakisi hiyo katika wigo uliokubalika kwa nchi za SADC na EAC wa chini ya asilimia 3.

 

MISAADA NA MIKOPO

Ndugu Wanahabari, Serikali katika vipindi tofauti imekua ikipokea misaada kutoka Wadau wa Maendeleo na Mashirika ya Fedha ya kimataifa kutokana na uwepo wa nakisi ya bajeti ili kugharamia utekelezaji wa bajeti kwa ufanisi. Aidha, utegemezi wa misaada na mikopo nafuu imeendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 20.7 ya bajeti yote katika miaka ya 2010/11 - 2014/15 hadi wastani wa asilimia 9.2 mwaka 2015/16 - 2019/20.  Kupungua kwa utegemezi katika misaada na mikopo nafuu kulitokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani. Aidha, kiasi cha mikopo kiliongezeka na kutoka shilingi bilioni 2,357.3 mwaka 2011/12 hadi shilingi bilioni 5,214.9 mwaka 2020/21. Kuongezeka kwa kiwango cha mikopo kulitokana na uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayochangia ukuaji wa uchumi. Hadi Juni 2021, deni la Serikali lilifikia shilingi bilioni 64,497.8 ikilinganishwa na bilioni 56,449.8 Juni 2020. Aidha, Serikali itaendelea kuhakikisha deni serikali linaendelea kuwa himilivu na mikopo inaelekezwa kwenye miradi yenye tija kwa Taifa.

 

IDADI YA WATU

Ndugu Wanahabari, idadi ya watu nchini imeendelea kuongezeka kila mwaka ambapo katika awamu ya kwanza (1966 -1985), wastani wa idadi ya watu ulikadiriwa kuwa milioni 16.1, awamu ya pili watu milioni 24.3, awamu ya tatu watu milioni 32.3 awamu ya nne watu milioni 42.4 na awamu ya tano watu milioni 51.8. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na viashiria muhimu vya mabadiliko ya idadi ya watu kama vifo na vizazi, Tanzania ilikadiriwa kuwa na watu milioni 57.6 mwaka 2020 ikilinganishwa na watu milioni 55.9 mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia 3.1.  Ni matumaini yetu kuwa sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022 itatoa idadi halisi ya watu nchini. Hivyo, nitumie fursa hii kuendelea kutoa rai kwa watanzania wote kushiriki katika zoezi la kuhesabiwa ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi.

 

Ndugu Wanahabari, kwa niaba ya Wizara ya Fedha na Mipango niwashukuru tena kwa ushirikiano wenu ambao mmekuwa mkiutoa pindi tunapowahitaji, na niwahakikishie kuwa Wizara itaendelea kufanya kazi nanyi bega kwa bega katika masuala yote ya kujenga uchumi wa Taifa letu ambayo wananchi wana haki ya kupata taarifa.

 

                                            KAZI IENDELEE

                                   Asanteni kwa kunisikiliza