Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TAARIFA KWA UMMA, DKT. MWAKIBINGA: LETENI MAONI YA MABORESHO YA SHERIA YA UNUNUZI

13 May, 2022
TAARIFA KWA UMMA, DKT. MWAKIBINGA: LETENI MAONI YA MABORESHO YA SHERIA YA UNUNUZI

TAARIFA KWA UMMA

DKT. MWAKIBINGA: LETENI MAONI YA MABORESHO YA SHERIA YA UNUNUZI

Wizara ya Fedha na Mipango imetoa wito kwa wadau wa sekta ya ununuzi wa umma nchini kutoa mawazo kuwezesha maboresho ya Sheria ya ununuzi wa umma ili kuleta tija kwa Serikali.

Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Frederick Mwakibinga, wakati akitoa elimu kuhusu sera, Sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi wa umma kwa washiriki waliotembelea banda la wizara hiyo, katika wiki ya ununuzi wa umma, jijini Arusha.

Alisema kuwa kuna Sheria ya ununuzi wa umma sura 410 na kanuni zake ambayo kwa mara ya mwisho ilipitiwa mwaka 2013 na kanuni zake kutoka mwaka 2016.

‘’Tunaendelea kukusanya maoni kutoka makundi mbalimbali na watu wote ambao wanadhani nini kifanyike ili Sheria iweze kutekelezeka na iweze kunufaisha nchi, hili ni jukumu letu kuhakikisha kuwa eneo la ununuzi wa umma lina sera, Sheria, kanuni na miongozo inayokuwa na tija kwa Taifa’’ alisema Dkt. Mwakibinga.

Alisema Sheria ya ununuzi wa umma inalinda maslahi ya Taifa kwani inawapa wananchi pamoja na wafadhili imani na Serikali katika matumizi ya fedha hivyo matumizi ya sheria hayapaswi kuingiliwa na mashinikizo.

Dkt. Mwakibinga alisisitiza maafisa manunuzi nchini kusimama katika sheria, kufanya kazi kwa nidhamu, kuheshimu taratibu za ununuzi na kuepuka kukiuka matumizi ya sheria kutokana na shinikizo lolote na kuwasiliana na wizara endapo watakutana na changamoto ya shinikizo la aina yoyote.

Aidha, Dkt. Mwakibinga alisema kuwa Wizara imetoa kanuni za maadili kwa wote wanaoshiriki katika ununuzi wa umma ili kuweza kuwajumuisha wote wanaoshiriki katika ununuzi wa umma kwa kuwa maamuzi yao huathiri ununuzi wa umma.

Akizungumza kuhusu wiki ya ununuzi wa umma alisema kuwa wiki hiyo ni ya muhimu katika kuelimisha umma katika masuala mbalimbali ya ununuzi wa umma ili kufahamu umuhimu wake.

Alisema kuwa matumizi ya teknolojia katika ununuzi wa umma yanahakikisha eneo hilo linaendeshwa kwa kujali maslahi ya Serikali na kushauri watendaji wote kuzingatia sheria, kanuni na kuzingatia maadili.

Kwa upande wao washiriki waliotembelea banda la Wizara hiyo walipongeza elimu inayotolewa katika wiki ya ununuzi wa umma na kutoa rai elimu kutolewa zaidi katika ngazi zote ili kuwezesha elimu hiyo kuongeza tija katika sekta ya ununuzi wa umma nchini.

Kongamano la Wiki ya ununuzi wa Umma limeandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini ambazo ni Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).

 

Imetolewa na:

Benny Mwaipaja

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha ya Mipango