Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

SERIKALI YAWATAKA WAKANDARASI KUTOA MAONI KUBORESHA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA

05 Nov, 2026
SERIKALI YAWATAKA WAKANDARASI KUTOA MAONI KUBORESHA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA

Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba,  akiagana na Mshauri wa  Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania, Bi. Umehani Khatri, baada ya kumalizika kwa Kikao cha Mapitio ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, kwa wakandarasi wakati wa kikao na wakandarasi wanaoshiriki katika ununuzi wa umma na ugavi, jijini Dar es Salaam.

 

Wakandarasi wazawa wametakiwa kutoa maoni na mapendekezo kuhusu changamoto zinazowakabili katika ununuzi wa umma ili kuwezesha Serikali kuboresha sheria, sera na miongozo ya ununuzi na ugavi kwa lengo la kuongeza ushiriki wao katika miradi ya maendeleo kuelekea Dira  2050.

Wito huo umetolewa na Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba, wakati wa kikao na wakandarasi kilicholenga kupata maoni kuhusu mapitio ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410.

Bw. Haraba amesema ununuzi wa umma ni nyenzo muhimu katika kuchochea uzalishaji wa ndani, kukuza biashara, kuongeza ajira na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi, hivyo ni muhimu kuboresha mfumo huo ili kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema pamoja na kuwepo kwa fursa za upendeleo wa kitaifa na kipekee kwa wazawa, upendeleo kwa bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na ushiriki wa kampuni za ndani kupitia ubia na mikataba midogo, bado kuna umuhimu wa kutathmini utekelezaji wake ili kubaini changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi.

Ameeleza kuwa mapitio hayo yanalenga pia kuimarisha fursa kwa wazawa, biashara ndogo na za kati, kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika michakato ya zabuni, kuboresha usimamizi wa mikataba na mifumo ya malipo kwa wakandarasi na watoa huduma. 

Kwa upande wake, Mshauri wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania, Bi. Umehani Khatri, amesema Washirika wa Maendeleo wakiwemo Ujerumani, Uswisi, Umoja wa Ulaya na GIZ wameunga mkono mchakato huo kupitia Mpango wa Good Financial Governance (GFG III). 

Amesema mpango huo unalenga kusaidia Serikali katika maeneo ya uhamasishaji wa mapato, udhibiti wa matumizi ya umma, kuimarisha uwazi katika sera za fedha na usimamizi wa fedha za umma. 

Ameeleza kuwa kuboresha mfumo wa ununuzi na ugavi ni sehemu muhimu ya juhudi hizo kwa kuwa unahusisha matumizi ya rasilimali za umma, hivyo ni muhimu kuhakikisha ununuzi unafanyika kwa uwazi, ufanisi na uwajibikaji. 

Kwa upande wao, wakandarasi wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuandaa jukwaa hilo lililowawezesha kueleza changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa Sheria za Ununuzi wa Umma.

Wamesema pamoja na nia ya Serikali ya kuwawezesha wakandarasi wazawa kunufaika na zabuni za umma, bado kuna changamoto katika utekelezaji wa fursa zilizowekwa, hivyo wametaka maoni na mapendekezo yao yazingatiwe katika maboresho ya sheria, sera na miongozo husika.

Wamesisitiza kuwa maboresho hayo yatasaidia kuongeza ushiriki wa wakandarasi wazawa katika miradi ya kimkakati, kukuza kampuni za ndani, kuongeza ajira na kujenga uwezo wa kitaalamu, sambamba na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na utekelezaji wa Dira 2050. 

Mwisho.