Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

SERIKALI YATHAMINI MCHANGO WA BENKI YA DUNIA KATIKA KUKUZA UCHUMI.

18 May, 2026
SERIKALI YATHAMINI MCHANGO WA BENKI YA DUNIA KATIKA KUKUZA UCHUMI.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali baada ya hafla ya  kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbambwe, Bw. Nathan Belete, baada ya kumaliza muda wake, iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt, jijini Dar es Salaam.

 

Serikali ya Tanzania imeeleza kuthamini mchango mkubwa wa Benki ya Dunia katika kuendeleza agenda ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi.

Hayo yameelezwa katika Hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) wakati wa hafla ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbambwe, Bw. Nathan Belete na kumkaribisha rasmi Bw. Firas Raad, aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo ambapo Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alikuwa mgeni rasmi.

Mhe. Munde alisema kuwa  ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Nampongeza Bw. Nathan Belete kwa kujitolea kwake na ushirikiano mzuri aliouonesha katika kipindi chake cha utumishi nchini Tanzania. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha pamoja na watumishi wa Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla tunamtakia mafanikio mema katika majukumu yake mapya ya baadaye”, alisema Mhe. Munde.

Aidha, alimkaribisha kwa moyo mkunjufu, Bw. Firas Raad, anayechukua nafasi ya Mkurugenzi huyo,  na kuahidi kuwa Wizara ya Fedha ipo tayari kufanya kazi kwa karibu naye katika kuendeleza vipaumbele vya pamoja vya maendeleo, ambapo Tanzania inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mhe. Munde alisema kuwa, uwepo wa Mhe.Waziri Mkuu katika hafla hiyo ni ishara ya namna Serikali inavyothamini ushirikiano wake na Benki ya Dunia pamoja na mchango wa washirika wa maendeleo katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia umekua kwa  kiwango kikubwa, hususan katika maeneo ya kimkakati ya maendeleo.

Alibainisha kuwa katika kipindi cha Mkurugenzi huyo takribani dola za Marekani bilioni 4.27 zilipatikana kupitia miradi na programu katika sekta mbalimbali ikiwemo usafirishaji, nishati, maji, kilimo, afya, elimu, maendeleo ya miji, hifadhi ya jamii, mageuzi ya sera pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema kuwa kwa ujumla hadi kufikia Aprili 30, 2026, thamani ya miradi ya Benki ya Dunia nchini Tanzania ilikuwa imefikia dola za Marekani bilioni 8.95. 

“Miradi hii imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya Watanzania pamoja na kuimarisha ajenda ya mageuzi ya uchumi wa nchi,” alisema Dkt. Mwamba.

Aidha Dkt. Mwamba  alisifu uwezo wa Bw. Belete katika kusimamia utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia muda, kuongeza kasi ya utoaji wa fedha, ufanisi wa taasisi na kuhakikisha matokeo yanayopimika yanafikiwa.

Naye  aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbambwe, Bw. Nathan Belete, alisema kuwa Benki ya Dunia inafurahishwa na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Serikali ya Tanzania katika kusukuma mbele ajenda ya mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya taifa.

Alisema kuwa ushirikiano huo umewezesha Tanzania kupata ongezeko kubwa la fedha za maendeleo kutoka Benki ya Dunia, hatua iliyosaidia kuharakisha utekelezaji wa mageuzi katika sekta mbalimbali muhimu.

Alieleza kuwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu, alikuwa mstari wa mbele kusisitiza umuhimu wa miradi mikubwa yenye matokeo ya kweli kwa maendeleo ya nchi, badala ya miradi midogo isiyoleta mabadiliko makubwa kiuchumi.

“Alikuwa akiniambia wazi kuwa Tanzania haiwezi kukua kwa ‘miradi ya maandazi na chapati’ na alisisitiza kuwa ili nchi iweze kusukuma mageuzi makubwa, ni lazima ipate uwekezaji mkubwa na wa maana,” alisema, Bw. Belete.

Bw. Belete alisema kuwa  Tanzania ilifanikiwa kuongeza kiwango cha fedha za msaada wa bajeti (DPO) kutoka dola milioni 250 hadi zaidi ya dola milioni 500 kwa mwaka, jambo lililowezesha kuanzishwa kwa mageuzi muhimu katika sekta ya elimu, maendeleo ya sekta binafsi pamoja na uwekezaji kupitia ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotumia vizuri zaidi fedha za Benki ya Dunia barani Afrika ambapo matokeo yanaonekana wazi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, nishati, uchukuzi na miundombinu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyene Nombo na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo.

Mwisho.