Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

SERIKALI YAHIMIZA WAHITIMU KUTUMIA ELIMU KAMA NYENZO YA KUJILETEA MAENDELEO

28 Nov, 2026
SERIKALI YAHIMIZA WAHITIMU KUTUMIA ELIMU KAMA NYENZO YA KUJILETEA MAENDELEO

Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Amina Makilagi  akizungumza katika Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Pili, kwa Mara ya 14, Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Mwanza, yaliyofanyika katika Kampasi ya Chuo hicho, jijini Mwanza, Novemba 27, 2026.

 

Serikali imewahimiza wahitimu wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Mwanza, kutumia elimu na ujuzi walioupata chuoni hapo kama nyenzo ya kujiletea maendeleo kwa kuanzisha shughuli za kiuchumi ili kuwawezesha kujiajiri.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Amina Makilagi kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, Duru ya Pili, kwa Mara ya 14, yaliyofanyika jijini Mwanza, Bi. Makilagi alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi, hasa vijana, kupata elimu, mitaji, teknolojia na masoko ili washiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

“ Wahitimu mnapaswa kutumia elimu na ujuzi mlioupata chuoni hapa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, kubuni fursa za kiuchumi na kuanzisha shughuli zitakazowawezesha kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine. Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo” alisema Mhe. Makilagi."

Mhe. Makilagi alieleza kuwa elimu na ujuzi wanaoupata wahitimu ni nyenzo muhimu katika kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii, hivyo wanapaswa  kubuni shughuli za uzalishaji, kuanzisha biashara na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yanayowazunguka  kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.

Aidha, alisema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ujasiriamali ili kuwawezesha wananchi kutumia maarifa na ujuzi walionao kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi. Alisisitiza kuwa, ushiriki wa wananchi katika shughuli za uzalishaji ni muhimu katika kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo endelevu ya Taifa.

Aliongeza kuwa, wahitimu wanapaswa kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira. Aliwataka kutumia fursa zilizopo kwa ubunifu na kuzingatia maadili, uwajibikaji na bidii katika kutekeleza majukumu yao.

Mhe. Makilagi alikipongeza Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini kwa kuendelea kutoa mafunzo yanayolenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii. Alisema mchango wa Chuo hicho ni muhimu katika kuandaa wataalamu wenye maarifa na ujuzi wa kuchochea maendeleo ya vijijini na Taifa kwa ujumla.

Alikihimiza Chuo hicho kuendelea kuboresha programu zake za mafunzo ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na changamoto za maendeleo, huku akiwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii. 

Mahafali hayo ya 40 ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, Duru ya Pili, kwa Mara ya 14, yamefanyika katika Kampasi ya Mwanza, yakitoa fursa ya kutambua mafanikio ya wahitimu katika kukamilisha mafunzo yao na kuwatia moyo kutumia elimu na ujuzi walioupata katika kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Mwisho.