Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

SERIKALI KUIMARISHA UPATIKANAJI WA MIKOPO KWA VIJANA

03 Nov, 2026
SERIKALI KUIMARISHA UPATIKANAJI WA MIKOPO KWA VIJANA

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akijibu maswali ya wabunge, bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

 

Serikali imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na benki za biashara nchini kuhamasisha uanzishwaji na upanuzi wa madirisha maalumu pamoja na bidhaa za mikopo zinazolenga kuwawezesha vijana kupata mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Timida Mpoki Fyadomo, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuanzisha dirisha maalumu la vijana katika benki za biashara nchini, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alisema Serikali inatambua umuhimu wa kuwawezesha vijana kupata mitaji.

Alisema Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za fedha kwa vijana kupitia benki na taasisi nyingine za fedha, akibainisha kuwa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaonesha kuwa mwaka 2025 akaunti za akiba za vijana katika benki zilifikia milioni 9.58.

“Serikali itaendelea kushirikiana na benki za biashara kuhamasisha uanzishwaji na upanuzi wa madirisha na bidhaa mahsusi za mikopo kwa vijana kwa lengo la kupunguza vikwazo vinavyowakabili vijana katika kupata huduma za kifedha, hususan mikopo ya kuwawezesha kujiajiri na kupanua shughuli zao za kiuchumi” alisema Mhe. Mhandisi Munde.

Alieleza kuwa Serikali imechukua hatua za kuimarisha mifumo ya udhamini wa mikopo, programu za uwezeshaji na elimu ya fedha ili kuongeza fursa za vijana kupata mitaji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

Alitaja hatua nyingine kuwa ni kutungwa kwa Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika, Na. 5 ya mwaka 2026, inayolenga kupunguza vikwazo vya dhamana kwa wanaohitaji mikopo.

Mhe. Munde aliongeza kuwa hatua hizo zinalenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa vijana ili waweze kuanzisha na kukuza biashara, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira.

Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za fedha ni sehemu muhimu ya kuimarisha mazingira ya vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia upatikanaji wa huduma za kifedha.

Akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Mhe. Kenneth Ernest Nollo, aliyetaka kujua lini Serikali itaanza utaratibu wa kutoa taarifa Bungeni kuhusu fedha zinazopatikana kutokana na migodi mikubwa ya madini, mafuta na gesi kila mwaka, Mhe. Munde alisema taarifa hizo tayari hutolewa kupitia njia mbalimbali, ikiwemo utaratibu ulioainishwa katika Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi.

Alifafanua kuwa kifungu cha 16(1) cha Sheria hiyo kinaielekeza Kamati ya TEITI kuchapisha taarifa ya kila mwaka inayoonesha ulinganifu wa mapato yote yanayolipwa na kampuni kubwa katika sekta ya uziduaji na yale yanayopokelewa na Serikali.

Aidha, alisema taarifa hizo pia huwasilishwa Bungeni na mawaziri wanaosimamia sekta husika wakati wa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zao.

“Serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa taarifa hizo kwa umma likiwemo Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuendeleza dhana ya uwazi na uwajibikaji” alisema Mhe. Mhandisi Munde.

Aliongeza kuwa taarifa hizo zitahusisha pia mapato yanayotokana na mfumo wa hisa za Serikali unaojulikana kama Free Carried Interest (FCI), unaopatikana kupitia kampuni zilizosaini mikataba ya haki za uchimbaji madini.
Hata hivyo hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za taifa na kuhakikisha mapato yanayotokana na uwekezaji katika sekta za madini mafuta na gesi yanawekwa wazi kwa Bunge na wananchi kwa ujumla.

Mwisho.