Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

RAIS SAMIA KUZINDUA SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA MNYORORO WA UGAVI JIJINI DODOMA.

04 Apr, 2026
RAIS SAMIA KUZINDUA SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA MNYORORO WA UGAVI JIJINI DODOMA.

Kaimu Kamishna, Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba, akizungumza wakati wa mkutano wa Wizara ya Fedha na Waandishi wa Habari, uliofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma ambapo alizungumzia kuhusu Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, unaotarajiwa kufanyika tarehe 08 Aprili 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, tarehe 08 Aprili 2026 katika Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre uliopo jijini Dodoma.

Hayo yalibainishwa na Kaimu Kamishna Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Alisema kuwa uzinduzi huo ni hatua muhimu ya kimkakati inayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.

‘‘Sera hii mpya imeandaliwa ili kuweka mfumo jumuishi na wa kimkakati wa kusimamia shughuli zote za mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma Mfumo huu unajumuisha hatua zote muhimu kuanzia upangaji wa mahitaji ununuzi wa umma, ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali, upokeaji, uhifadhi, usambazaji hadi uondoshaji wa mali za umma zilizochakaa,’’alisema Bw. Haraba.

Alisema kuwa sera hiyo inalenga kuleta mapinduzi katika kuimarisha uwazi uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika kila mradi au huduma.

Bw. Haraba alieleza kuwa, Sera hiyo inalenga kuunganisha shughuli za mnyororo wa ugavi ambazo awali zilikuwa zikitekelezwa kupitia Sheria na Mifumo mbalimbali bila kuwa na mwongozo mmoja wa kisera

‘’Sera hii pia inalenga kukuza matumizi ya teknolojia na utawala bora katika kusimamia rasilimali za Taifa, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na makundi maalumu ya kijamii ili kupanua wigo wa fursa za kiuchumi na ajira kwa Watanzania’’, alieleza Bw. Haraba.

Aliongeza kuwa, Sera hiyo pia itachochea ukuaji wa viwanda vya ndani kwa kuhimiza matumizi ya rasilimali na malighafi zinazopatikana nchini hatua itakayoongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania kimataifa.

Aliongeza kuwa, mwelekeo huu mpya unaendana na maono ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara na shindani huku ukiongeza thamani ya rasilimali za ndani kwa faida ya wananchi wote.

Bw. Haraba alitoa wito kwa wadau wote na wananchi kwa ujumla kushiriki katika hafla hiyo muhimu itakayoweka msingi mpya wa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kote nchini.

MWISHO.