Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

MKUTANO WA MWAKA WA BARAZA LA MAWAZIRI NA MKUTANO WA MAAFISA WAANDAMIZI WA ESAAMLG WAFUNGULIWA KIGALI-RWANDA.

05 Sep, 2026
MKUTANO WA MWAKA WA BARAZA LA MAWAZIRI NA MKUTANO WA MAAFISA WAANDAMIZI WA ESAAMLG WAFUNGULIWA KIGALI-RWANDA.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)(kulia), Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Juma Homera (Mb) (kushoto) na Naibu Gavana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Rwanda, Bw. Nick Barigye, wakiwa katika picha wakati wa hafla ya ufunguzi wa mikutano ya Mwaka ya Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kupambana na Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi (ESAAMLG), iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, Jijini Kigali nchini Rwanda.

 

Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar akiwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Homera, na Viongozi wengine wa Serikali wameshiriki ufunguzi wa mikutano ya Mwaka ya Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kupambana na Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi (ESAAMLG), uliofanyika leo tarehe 4 Septemba 2026, katika Hoteli ya Serena, Jijini Kigali nchini Rwanda.


Mikutano hiyo inajumuisha Mkutano wa 52 wa Maafisa Waandamizi na Mkutano wa 26 wa Baraza la Mawaziri, pamoja na Mkutano wa 9 wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.


Mikutano hii imewakutanisha viongozi wa Serikali katika ngazi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Fedha, Katiba na Sheria, Mambo ya Ndani na maafisa waandamizi kutoka nchi wanachama wa Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika lengo likiwa kuimarisha juhudi za pamoja za kupambana na utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi, na ufadhili wa silaha za maangamizi. 

Kauli mbiu ya mikutano ya mwaka huu inalenga kuweka msukumo wa kutoka kwenye kufuata matakwa ya kiufundi kwenda kwenye kuonesha matokeo halisi katika mifumo ya kupambana na uhalifu wa kifedha ndani ya ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Wakizunguza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, viongozi mbalimbali walielezea changamoto ya kuongezeka kwa tishio la utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na silaha za maangamizi na kutoa wito kwa nchi wanachama wa ESAAMLG kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kuongeza uwazi na usalama wa sekta ya fedha.


Ushiriki wa Tanzania katika Mikutano hii utaongeza ushirikiano kati yake na nchi nyingine wanachama katika masuala ya uchunguzi wa miamala shuku, ufuatiliaji wa fedha haramu na ujenzi wa mazingira salama ya biashara na uwekezaji hivyo kukuza imani ya wawekezaji na kuimarisha maendeleo ya uchumi na kijamii.

.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa maazimio na mapendekezo yatakayosaidia nchi wanachama kuimarisha sera, sheria na mifumo ya taasisi zao kwa lengo la kulinda uchumi wa mataifa yao dhidi ya matumizi haramu ya mifumo ya kifedha.

Viongozi wengine kutoka Tanzania walioshiriki ufunguzi huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, Kamishna wa Kitengo cha FIU, Bw. Majaba Magana, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bi. Sauda Msemo, wakuu wa taasisi, wataalamu wa sekta ya fedha, wasimamizi wa taasisi za kifedha na wadau wengine wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali za ukanda huo.

MWISHO