Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

MHE. MUNDE ATOA AGIZO KWA MKURUGENZI WILAYA YA NGORONGORO KUDHIBITI MAENEO YA KIMKAKATI.

12 Oct, 2026
MHE. MUNDE ATOA AGIZO KWA MKURUGENZI WILAYA YA NGORONGORO KUDHIBITI MAENEO YA KIMKAKATI.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Luteni Kanali Robert Augustino Kakomangile (wa pili kushoto),  Mbunge wa Ngorongoro, Mhe. Yannick Ndoinyo(wa pili kulia) na viongozi wengine kutoka Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Wilaya ya Ngorongoro baada ya kumalizika kwa ziara Wilayani hapo. 

 

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) amemuagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro kuhakikisha maeneo yanapangwa kuzingatia mahitaji ya sasa na mipango ya maendeleo ya baadaye hususani katika maeneo ya mpaka kati ya Tanzania na Kenya yaliyopo katika Wilaya hiyo.

Agizo hilo amelitoa wakati akihitimisha ziara ya kikazi Wilayani ya Ngorongoro, kufuatia ombi la Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Yannick Ndoinyo kupendekeza uhitaji wa Kituo cha kutoa huduma za Forodha katika Tarafa ya Loliondo na Sale Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha.

Mhe. Munde alieleza wasiwasi kuhusu wananchi ambao tayari wameanza kuanzisha makazi na shughuli za biashara katika maeneo yaliyotajwa kuwa na umuhimu wa kimkakati wa kujenga Kitui cha Forodha iwapo yatakidhi vigezo vya kisheria.

“Maeneo ya kimkakati yanapaswa kupangwa mapema ili kuzuia ujenzi holela ambao unaweza kuathiri mipango ya Serikali ya baadaye, maeneo haya yasikaliwe kiholela”, alisema Mhe. Munde.

Mhe. Munde alisisitiza umuhimu wa kuwa na mpango mpana wa matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro, akisema wilaya hiyo ni kubwa na inaendelea kukua na pia mipango endelevu ni sehemu ya kivutio cha uwekezaji.

Alieleza kuwa Wilaya ya Ngorongoro ina fursa nyingi za kiuchumi na kimkakati ambazo zikisimamiwa na kupangwa vizuri zinaweza kuchochea maendeleo ya eneo hilo na kuboresha maisha ya wananchi.

Akizungumza kuhusu changamoto zinazopatikana katika maeneo ya mipakani, alisema hazipaswi kuonekana kama vikwazo pekee, bali zinaweza kubadilishwa kuwa fursa za maendeleo endapo zitatatuliwa kwa mipango madhubuti.

Alisema Serikali imepokea hoja na mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa wananchi, akiwemo Mbunge, kuhusu namna ya kutumia fursa zilizopo Ngorongoro katika kuboresha huduma na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Kiongozi huyo alisema wataalamu wamepewa jukumu la kuchambua maeneo ya.    yaliyopendekezwa kuwa na kituo cha  Forodha na maamuzi yatazingatia maslahi ya Serikali pamoja na wananchi wanaoishi katika maeneo husika.

“Wataalamu wetu wameelekezwa kwenda kuyachambua na kuyatafiti maeneo hayo ili hatimaye tufikie muafaka kuhusu hatua gani inapaswa kuchukuliwa,” alisema Mhe. Munde.

Katika hatua nyingine, Kamishna wa Uhamiaji anaeshughulikia Divisheni ya mipaka ameagizwa kuimarisha udhibiti katika maeneo ya mpakani wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kufanya uamuzi kuhusu eneo la kituo cha Forodha.

Kiongozi huyo alisema taarifa zilizotolewa wakati wa ziara zinaonyesha kuwa siku za Jumatatu kuna ongezeko la shughuli za kiuchumi na mwingiliano wa watu katika eneo hilo, hivyo inapaswa kuwa fursa kwa mamlaka husika kwenda kujionea hali halisi na kubaini hatua zinazohitajika ili kuimarisha udhibiti.

Kwa upande wao Viongozi walioambatana na Mhe. Munde, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Luteni Kanali Robert Augustino Kakomangile, wajumbe kutoka Uhamiaji na Mamalaka ya Mapato Tanzania wameahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa  ili kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa mipango ya Maendeleo.

Wamemshukuru Mheshimiwa Munde kwa kufika katika eneo hilo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa Mbunge wa Ngorongoro katia vikao vya Bunge, jijini Dodoma la kujionea uhitaji wa Kituo cha huduma za Forodha.

Naibu Waziri Mhe. Munde alitembelea maeneo ya mpakani katika Kijiji cha Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo, pamoja na Kijiji cha Olmiti, Kata ya Enguserosambu, Tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha 

Mwisho.