Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

MHE BALOZI OMAR ASISITIZA UWEKEZAJI KATIKA MAANDALIZI YA MIRADI KUVUTIA MITAJI AFRIKA

28 Nov, 2026
MHE BALOZI OMAR ASISITIZA UWEKEZAJI KATIKA MAANDALIZI YA MIRADI KUVUTIA MITAJI AFRIKA

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar akizungumza  jijini Paris nchini Ufaransa, wakati akichangia mada kuhusu Usanifu Mpya wa Kifedha wa Afrika kwa Maendeleo (NAFAD), kama chanzo mbadala cha fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo katika nchi za Bara la Afrika, ulifanyika kando ya Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi kwa ajili ya Afrika, ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Ushirikino wa Kiuchumi na Maendeleo la Ufaransa-OECD, ukilenga kuimarisha mfumo wa kifedha wa Afrika ili mitaji ielekezwe kwa ufanisi zaidi katika vipaumbele vya maendeleo ya Bara la Afrika.

 

Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa uandaaji wa miradi inayoweza kuvutia mitaji na uwekezaji ni changamoto inayozikabili nchi nyingi za Afrika kuyaikia masoko ya mitaji na dhamana.

Mhe. Balozi Omar amesema hayo jijini Paris nchini Ufaransa, wakati akichangia mada kuhusu Usanifu Mpya wa Kifedha wa Afrika kwa Maendeleo (NAFAD), kama chanzo mbadala cha fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo katika nchi za Bara la Afrika, ukiwaleta pamoja wawakilishi wa ngazi ya juu wa nchi za Afrika na OECD, taasisi za ufadhili wa maendeleo na wadau wengine wa kifedha.

Afrika ina rasilimali nyingi za kifedha, zikiwemo akiba za ndani za muda mrefu zinazokadiriwa kuwa takriban dola za Marekani trilioni 4, huku sehemu kubwa ya rasilimali hizo bado haielekezwi vya kutosha katika uwekezaji wa uzalishaji, wakati bara hilo linaendelea kukabiliana na pengo la ufadhili wa maendeleo linalokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni 400 kwa mwaka.

Usanifu huu unalenga kukabiliana na changamoto hizo kwa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa taasisi za kifedha za Afrika na kutumia uwezo, mizania, rasilimali na zana zao kuhamasisha ufadhili wa ziada.

Unahusisha taasisi za ufadhili wa maendeleo za kitaifa na kikanda, benki za biashara, mifuko ya pensheni, taasisi za bima, masoko ya mitaji, serikali, washirika wa maendeleo na wawekezaji wa sekta binafsi, kwa lengo la kuboresha uratibu, kuwezesha uhamasishaji wa mitaji ya taasisi na kuimarisha uwezo wa taasisi za kifedha kufadhili uwekezaji wa maendeleo.

Katika mchango wake, Mhe. Balozi Omar alitaja maandalizi ya miradi kama kikwazo kikubwa, akisema kuwa pengo katika masoko mengi si ukosefu wa mtaji, bali ni uhaba wa miradi inayokopesheka na kusisitiza kuwekeza katika maandalizi ya miradi ili kuhakikisha miradi iko tayari kwa ufadhili wa soko.

Mhe. Balozi Omar alifafanua hali ya akiba ya ndani, akibainisha kuwa mifuko ya pensheni na bima, kwa mfano, inaongozwa na wajibu wa uaminifu na kwa kawaida hushikilia mali za ndani za muda mfupi na kuonya kuwa matarajio kuhusu akiba ya ndani lazima yadhibitiwe kwa uangalifu, hasa katika masoko madogo.

Akizungumzia kuhusu vihatarishi vya kifedha, alisisitiza hatari za madeni ya dharura, hasa dhamana za serikali na  kutoa wito wa kusajili dhamana zote kwa upande wa madeni na fedha.

Aidha, Mhe. Balozi Omar alipendekeza kuwa viwango vya nchi vya uwezo wa kukopesheka katika masoko ya kimataifa na dhamana, vinavyotolewa na mashirika kama Moody's na Fitch ni muhimu vitumike  kwa ajili ya kuendesha bei ya dhamana hizo.

Mjadala huo ulifanyika kando ya Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi kwa ajili ya Afrika, ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Ushirikino wa Kiuchumi na Maendeleo la Ufaransa-OECD, ukilenga kuimarisha mfumo wa kifedha wa Afrika ili mitaji ielekezwe kwa ufanisi zaidi katika vipaumbele vya maendeleo ya Bara.

Aidha, NAFAD uliandaliwa kukabiliana na changamoto za kimuundo zinazoathiri mazingira ya ufadhili wa maendeleo barani Afrika, zikiwemo gharama kubwa ya mtaji, masoko ya kifedha yaliyogawanyika, uhamasishaji mdogo wa rasilimali za ndani na uratibu hafifu miongoni mwa taasisi za kifedha.

Mwisho