Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

MAPITIO YA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA KUCHOCHEA UCHUMI WA NDANI

05 Nov, 2026
MAPITIO YA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA KUCHOCHEA UCHUMI WA NDANI

Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba (katikati) na Mshauri wa  Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania, Bi. Umehani Khetri (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na wadau wanaoshiriki katika ununuzi wa umma na ugavi, jijini Dar es Salaam.

 

Serikali imesema mapitio ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, yanalenga kuimarisha ushiriki wa wazawa na kampuni za ndani katika ununuzi wa umma, kukuza biashara na uzalishaji wa ndani pamoja na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za umma kwa kuzingatia Dira 2050.

Hayo yamesemwa na Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba, wakati wa kikao na wadau wanaoshiriki katika ununuzi wa umma na ugavi, kilicholenga kupata maoni na mapendekezo kuhusu mapitio ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Bw. Haraba amesema ununuzi wa umma una nafasi muhimu katika kufikia malengo ya Dira  2050, hususan katika kuchochea uzalishaji wa ndani, kukuza biashara, kuongeza ajira na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Amesema mapitio hayo yanafanyika katika kipindi ambacho Serikali imeweka msukumo mkubwa katika kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na kukuza sekta binafsi.

“Katika kufikia malengo hayo, ununuzi wa umma una nafasi kubwa kwa sababu ni miongoni mwa njia ambazo Serikali inaweza kutumia kuchochea uzalishaji wa ndani, kukuza biashara, kuongeza ajira na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi,” amesema Bw. Haraba.

Bw. Haraba amesema kuwa Serikali imeweka msingi wa kuimarisha usimamizi wa mnyororo wa ugavi kupitia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 pamoja na Mkakati wake wa Utekelezaji wa mwaka 2025 hadi 2035.

Akizungumzia mfumo wa sasa wa kisheria, Bw. Haraba amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, Toleo la mwaka 2023, pamoja na Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024 na marekebisho yake, zimeweka masharti mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushiriki wa wazawa katika shughuli za ununuzi wa umma.

Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na upendeleo wa kitaifa na upendeleo wa kipekee kwa wazawa, upendeleo kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, pamoja na fursa kwa kampuni za ndani kushiriki katika utekelezaji wa mikataba kupitia ubia na mikataba midogo.

Hata hivyo, amesema ni muhimu kutathmini namna fursa hizo zinavyotekelezwa ili kubaini kama zinawanufaisha ipasavyo wazalishaji, wazabuni, wakandarasi na watoa huduma wa ndani.

 “Ni muhimu kusikiliza uzoefu wa wadau, kubaini changamoto za kisheria na kiutendaji na kupata mapendekezo ya kuboresha mfumo uliopo ili kuongeza ushiriki wa wazawa, kukuza biashara za ndani na kuimarisha ushindani wa haki katika ununuzi wa umma,” amesema.

Amesema kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha mabadiliko yanayopendekezwa katika sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yanaakisi mahitaji halisi ya wadau wanaoshiriki katika mfumo wa ununuzi wa umma na ugavi.

Kwa mujibu wa Bw. Haraba, maeneo yanayotarajiwa kujadiliwa ni pamoja na namna ya kuongeza ushiriki wa wazawa na kampuni za ndani, kuimarisha fursa kwa wazalishaji na biashara ndogo na za kati, kuboresha matumizi ya upendeleo, ubia na mikataba midogo, pamoja na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika michakato ya zabuni.

Amesema maoni na mapendekezo yatakayopatikana kutoka kwa wadau yatasaidia Serikali kuandaa mfumo wa ununuzi wa umma na ugavi unaowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

“Tunaamini kuwa Mfumo mzuri ununuzi wa umma na ugavi unaweka msingi imara unaozingatia uwazi, ufanisi, ushindani wa haki, thamani halisi ya fedha na matumizi bora ya rasilimali za ndani, sambamba na kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira 2050,” amesema Bw. Haraba.

Mapitio hayo yanatarajiwa kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kutoa uzoefu, changamoto na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya ununuzi wa umma na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa ndani.

Kwa upande wake Mshauri wa  Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania, Bi. Umehani Khetri, ambaye Shirika lake linafadhili sehemu ya vikao vya wadau wa ununuzi alisema kuwa suala la ununuzi ni muhimu katika maendeleo.

Amesema kuwa anapongeza hatua ya kuwakutanisha wadau kutoa maoni jambo amabalo linaongeza uwazi na kuwa na Mifumo shirikishi katika kuchochea maendeleo.

Mwisho.