Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

LWANGILI AIPONGEZA WIZARA YA FEDHA KWA KUTUMIA CAPITAL CITY MARATHON KUFIKISHA ELIMU YA FEDHA KWA WANANCHI

02 Nov, 2026
LWANGILI AIPONGEZA WIZARA YA FEDHA KWA KUTUMIA CAPITAL CITY MARATHON KUFIKISHA ELIMU YA FEDHA KWA WANANCHI

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda (katikati), akifurahia pamoja na watumishi wa Wizara hiyo walioonesha medali zao baada ya kukamilisha mbio za kilomita 21 katika Capital City Marathon katika Viwanja vya Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), jijini Dodoma, Novemba 1, 2026.

 

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kutumia mbio za Capital City Marathon (CaCiMa) kama jukwaa la kuwafikishia wananchi elimu ya fedha, akieleza kuwa majukwaa ya aina hiyo yana nafasi muhimu katika kuwafikia watu wa makundi mbalimbali na kuwajengea uwezo wa kusimamia rasilimali zao.

Bi. Lwangili ametoa kauli hiyo wakati wa mbio hizo zilizofanyika katika Viwanja vya Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), jijini Dodoma, kuanzia Oktoba 31 hadi Novemba 1, 2026, ambapo Wizara ya Fedha ilishiriki kwa kutoa elimu kupitia wataalamu wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha na Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali.

Kupitia ushiriki huo, elimu ya fedha ilitolewa kwa washiriki wa mbio, wajasiriamali, wafanyabiashara na wanachuo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ikilenga kuwajengea uwezo wa kuandaa bajeti, kusimamia mapato na matumizi, kuweka akiba na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.

Washiriki pia walielimishwa kuhusu fursa za uwekezaji kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja inayosimamiwa na UTT AMIS, namna ya kutathmini hatari na faida za uwekezaji, matumizi sahihi ya mikopo na kuepuka mikopo umiza. Elimu hiyo ilihusisha pia umuhimu wa bima katika kulinda afya, mali na biashara pamoja na maandalizi ya kifedha kwa maisha baada ya kustaafu.

Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa watumishi wa umma katika mbio hizo, Bi. Lwangili alisema kufanya mazoezi ni sehemu ya maandalizi ya kuwa na watumishi wenye afya bora na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Lengo letu kama Utumishi wa Umma ni kuhakikisha watumishi wanashiriki katika hamasa mbalimbali za mazoezi ili kujiweka sawa, kujenga afya njema na kuweza kuwahudumia wananchi vizuri zaidi. Tunapoendelea kutekeleza Dira 2050, ni muhimu kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi kwa faida ya afya zao na Taifa letu,” alisema Bi. Lwangili.

Aliongeza kuwa ushiriki wa pamoja katika shughuli hizo unasaidia kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza na kuchangia juhudi za kuboresha huduma za afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, alisema Capital City Marathon imekuwa fursa ya kuimarisha afya, kujenga mahusiano na kuwaunganisha washiriki kutoka makundi mbalimbali ya jamii.

“Mbio hizi zimekuwa fursa nzuri ya kuimarisha afya na kujenga mahusiano kati ya washiriki na zinatuwezesha kukutana na watu wengine kutoka katika jamii. Jambo lingine la kufurahisha ni kuona familia zikishiriki, wakiwemo watoto wadogo, jambo linalosaidia kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi tangu wakiwa na umri mdogo,” alisema Bw. Mwenda.

Ushiriki wa Wizara ya Fedha katika CaCiMa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Elimu kwa Umma kuhusu Masuala ya Fedha, unaolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, uwekezaji na matumizi ya huduma za kifedha ili kuwawezesha kufanya maamuzi yenye tija na kujenga ustawi wa kiuchumi.

MWISHO