Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

KOREA YAIPATIA TANZANIA BILIONI 441 ZA KUJENGA CHUO MAHIRI CHA TEHAMA DODOMA

05 Nov, 2026
KOREA YAIPATIA TANZANIA BILIONI 441 ZA KUJENGA CHUO MAHIRI CHA TEHAMA DODOMA

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, na Mkurugenzi Mtendaji Mwandamizi, Benki ya Exim ya Korea; Bw. Dong-Hoon Lee, wakisaini Hati za makubaliano ya Mkopo wenye masharti nafuu wa takribani dola za Marekani milioni 167.37, sawa na takribani shilingi za Tanzania bilioni 441.12, kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (Digital Technology Institute – DTI, jijini Dodoma, hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
 

 

TANZANIA inatarajia kupata Chuo Mahiri cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (DTI) jijini Dodoma, ambacho ujenzi wake unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 441, kupitia mkopo nafuu kutoka Serikali ya Korea Kusini, kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika teknolojia za kidijiti, ikiwemo Akili Unde.

Mradi huo utaanza kutekelezwa baada ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Exim ya Korea Kusini, Novemba 3 mwaka huu, kutia saini mkataba wa mkopo wenye riba nafuu wa dola za Marekani milioni 167.4, sawa na sh. bilioni 441.12, utakaotolewa kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea (EDCF).

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo, Jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alisema chuo hicho kitakuwa na mchango mkubwa katika kuandaa na kukuza wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika fani za kiufundi na kuimarisha sekta ya tehama nchini.

Alisema chuo hicho kitakuwa na vituo vya kisasa vya mafunzo, maabara, miundombinu ya kidijiti na tafiti, huku kikiimarisha uhusiano kati ya taasisi za elimu na sekta ya viwanda ili kupunguza pengo la ujuzi na kuchochea maendeleo ya teknolojia.

“Mradi huu umekuja wakati mwafaka ambapo Tanzania inaendelea kutekeleza ajenda ya mageuzi ya kidijiti na kujenga rasilimali watu pamoja na uwezo wa kitaasisi unaohitajika kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijiti’ Alisema Dkt. Mwamba.

Alisema Wizara ya Fedha itashirikiana kwa karibu na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo kutoa mchango wa ndani unaohitajika ili kuhakikisha unatekelezwa kwaufanisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mwandamizi wa Benki ya Exim ya Korea, Bw. Dong-Hoon Lee, alisema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa nchi hizo mbili kwa kuwa ni mradi wa kwanza wa EDCF kuidhinishwa mwaka huu na wa kwanza unaohusisha usaidizi katika eneo la Akili Unde.

Alisema majadiliano ya kuidhinisha mradi huo yalianza Aprili mwaka huu kisha ikatolewa sera ya usaidizi wa serikali Agosti mwaka huu na kufikia hatua hiyo ya utiaji saini mkataba huo Novemba mwaka huu.

Alisema kasi hiyo imetokana na ushirikiano thabiti kutoka Serikali ya Tanzania na kusisitiza kuwa Korea itaendelea kuwa mshirika wa kuaminika katika kusaidia maendeleo ya Tanzania kupitia miradi mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za barabara, nishati na afya.
“Ushirikiano huu utaimarisha ukuaji wa pande zote mbili na urafiki wa nchi hizi mbili” alisisitiza Bw. Lee.

Mradi huo wa Chuo Mahiri cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-Dodoma, unaongezwa katika orodha ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Exim ya Korea, yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.12, inayohusisha sekta za nishati, kilimo, maji safi na maji taka, reli na sekta nyinginezo.

Mwisho