Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

IMF YAFANYA MAJADILIANO NA TANZANIA KUHUSU USHIRIKIANO WA MAENDELEO

03 May, 2024
IMF YAFANYA MAJADILIANO NA TANZANIA KUHUSU USHIRIKIANO WA MAENDELEO
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amefungua vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) waliowasili nchini kwa ajili ya kufanya tathimini ili Tanzania iweze kupata fedha za awamu ya nne kupitia program ya Extended Credit Facility-(ECF), itakayowezesha kuendelea kuchachua na kuimarisha uchumi kupitia sekta za uzalishaji.
 
Kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma kimehusisha timu ya wataalamu kutoka IMF walioongozwa na Bw. Harris Charalambos Tsangarides waliokuja kufanya tathmini na pia kujadili namna ya kuiwezesha Tanzania kupata fedha ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha lake la Resilient and Sustainable Trust (RST).
 
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania inashukuru kwa msaada wa kiasi cha dola za Marekani milioni 455.3 zilizotolewa kwa awamu tatu za kwanza kati ya dola bilioni 1.1 ili kutekeleza miradi inayosaidia kuchochea maendeleo ya wananchi, kukuza uchumi jumuishi na kuiwezesha nchi kuhimili misukosuko ya kiuchumi inayoikabili dunia
 
“Tunaendelea kufanya kazi na wenzetu wa IMF kupitia programu ya ECF na sasa wamekuja kwenye misheni ya kusaidia Tanzania kuweza kunufaika na dirisha la Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi, programu hiyo ni mwendelezo wa programu za Shirika hilo za kuimarisha uchumi wa nchi wanachama wa Shirika hilo baada ya athari za Uviko 19.“, alieleza Mhe. Dkt. Nchemba
 
Dkt. Nchemba amelihakikishia IMF kuwa Tanzania itaendelea kutumia fedha zilizotolewa kulingana na makubaliano yaliyopo na pia amewapongeza kwa uamuzi wa kutembelea vivutio kama Ngorongoro na amewaomba wakipata nafasi waweze kutembelea maeneo mengine kama Serengeti, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar.
 
Alisema kuwa baada ya majadiliano na timu hiyo ya wataalam wa IMF Tanzania itapata sifa ya kuingia kwenye programu hiyo ya kunufaika na Mfuko wa RST ambapo kwa sasa haina vigezo hivyo.
 
Dkt. Nchemba aliishukuru IMF kwa niaba ya Serikali kwa msaada wake na miongozo katika utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF) kwa kuwa wamefanya jitihada kubwa katika kuhakikisha Tanzania inakidhi vigezo vya kupata fedha kutoka ECF kwa ajili ya kusaidia bajeti na changamoto zinazotokea duniani.
 
Alisema maeneo ambayo IMF imekuwa ikishirikiana na Tanzania yanaenda sambamba na ajenda ya Serikali ambayo inakusudia kutengeneza mazingira bora ya sekta ya uzalishaji ambayo kimsingi ni maeneo ambayo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayapa kipaumbele.
 
Mhe. Dkt. Nchemba alieleza kuwa maeneo hayo kwa muda mrefu yanatoa majawabu kwa matatizo yanayowakabili watanzania, yakiwemo matatizo ya ajira, kupunguza umasikini na kuwajengea uwezo watanzania kwa kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji.
 
Alisema kuwa Serikali ipo tayari kwa majadiliano, ambapo timu ya Wizara ya Fedha na taasisi zake itaanza katika majadiliano hayo na pia itaratibu majadiliano na Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira na wizara nyingine za kisekta.
 
Kwa upande wake Kiongozi wa Timu hiyo ya IMF Bw. Harris Charalambos Tsangarides, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza kwa umahili mpango wa ECF na kutimiza vigezo vilivyoweka katika mpango huo kwa wakati na kusaidia nchi kupata  kiasi cha dola za Marekani 455.3. 
 
Amesema majadiliano hayo ni mwendelezo wa mjadala uliofanyika katika Mikutano ya Majira ya Kipupwe yaliyofanyika jijini Washngton D.C, Marekani, ambapo Tanzania iliwasilisha maombi ya kutaka kunufaika na dirisha lake la Resilient and Sustainable Trust (RST) ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo wamekuja ili kufanya tathimini kwa kujadiliana na wadau namna ya kutekeleza maombi hayo.
 
Alisema kuwa baada ya majadiliano hayo watawasilisha hoja kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo kwa ajili ya kupitia ma kujadili mapendekezo yatakayotolewa.
 
Hali kadhalika Bw. Tsangarides  aliahidi kuendekleza ushirikiano wa karibu kati ya IMF na Tanzania.