Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

FUNGU 50 WIZARA YA FEDHA MSHINDI WA KWANZA MFULULIZO UANDAAJI BORA HESABU

27 Nov, 2026
FUNGU 50 WIZARA YA FEDHA MSHINDI WA KWANZA MFULULIZO UANDAAJI BORA HESABU

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, anayeshughulikia Huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua akipokea Tuzo ya mshindi wa kwanza wa uandaaji  bora wa hesabu kwa mwaka wa Fedha ulioishia 30 Juni 2025 katika kundi la Wizara na Idara za Serikali zinazojitegemea kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA Prof. Sylvia Shayo Temu,  jijini Dar es Salaam.

 

Wizara ya Fedha Fungu 50 Huduma za Hazina, imeibuka mshindi wa kwanza na kufanikiwa kupata tuzo ya waandaji bora wa hesabu kwa Mwaka wa Fedha ulioishia 30 Juni 2025 inayotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Tanzania (NBAA) katika kundi la Wizara na Idara za Serikali zinazojitegemea.

Akizungumza katika hafla hiyo ya utoaji tuzo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Huduma za Hazina ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Bw. Nsubili Joshua amesema kuwa ushindi unaopatikana katika mashindano ya kitaaluma yanayohusisha masuala ya uhasibu na usimamizi wa fedha ni ishara ya ubora, weledi na uwezo wa wataalamu wanaotoka katika taasisi zilizo chini ya Wizara.

Bw. Joshua amesema kuwa mafanikio hayo si ya mara ya kwanza, bali yamekuwa yakijitokeza kwa miaka mingi, jambo linaloonesha kuwa wataalamu wa masuala ya fedha na uhasibu wameendelea kuwa na uwezo mkubwa kitaaluma.

“Ushindi katika mashindano haya ni kiashiria kizuri kwa Wizara ya Fedha, kwani unaonesha ubora wa wataalamu wake katika utunzaji wa hesabu, usimamizi wa fedha na masuala ya ukaguzi”, alisema Bw. Joshua 

Aidha, amesema kuwa mafanikio hayo yanatoa taswira nzuri kwa Wizara ya Fedha, kwa kuwa washiriki kutoka taasisi mbalimbali za Wizara wameibuka washindi katika mashindano hayo, akiwemo mshindi wa jumla, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa Fungu 50, Wizara ya Fedha, CPA Nuru Abdallahmed, amesema mafanikio ya Wizara hiyo katika mashindano ya utayarishaji na usimamizi wa taarifa za fedha yametokana na ushirikiano, mshikamano na kujituma kwa viongozi pamoja na watumishi wa Wizara.

Amesema kuwa tangu aanze kusimamia Fungu 50, wamefanikiwa kushinda mara sita, wakishika nafasi ya kwanza mara tatu, nafasi ya pili mara mbili na nafasi ya tatu mara moja.

Amesema mafanikio hayo ni ya kujivunia, kwani mashindano hayo hushirikisha wizara mbalimbali zenye uwezo na weledi katika masuala ya usimamizi wa fedha, hivyo kufanya ushindani kuwa mkubwa. 

“Mashindano ya mwaka huu, Wizara ya Fedha imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza, ikiwa ni mara ya pili mfululizo baada ya kupata ushindi pia mwaka uliopita, jambo linaloonesha uwezo wa kudumisha kiwango cha utendaji na ubora katika usimamizi wa fedha za Serikali”, amesema CPA Abdallahmed. 

Aidha, amesema kudumisha ushindi kwa miaka mfululizo si jambo rahisi, bali kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya viongozi, watumishi na wadau wote wanaohusika na usimamizi, utunzaji na utayarishaji wa taarifa za fedha. 

CPA Abdallahmed amewashukuru viongozi wa Wizara, watumishi walio chini ya usimamizi wake pamoja na watendaji wanaohusika na masuala ya uhasibu kwa mchango wao katika kufanikisha mafanikio hayo. 

Awali akizungumza katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu, Bw. Nsubili Joshua alisema kuwa ni muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ubora wa taarifa za fedha, ikieleza kuwa taarifa hizo ni nyenzo muhimu katika kujenga taasisi imara na kufanikisha malengo ya Dira 2050.

“Taarifa za fedha zilizo sahihi na zenye uwazi huimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma, huongeza imani ya wawekezaji, hurahisisha kufanya maamuzi sahihi ya kiuchumi na huchochea maendeleo ya taasisi imara na endelevu” alisema Bw. Joshua.

Katika Kundi la Wizara na Idara za Serikali zinazojitegemea  Mshindi wa Pili alikuwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali. Aidha Mshindi wa Jumla katika Makundi 25 yaliyoshindanishwa, mshindi wa Jumla alikuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). 

Mwisho.