Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

FEDHA ZILIZOPO KWENYE MASHAURI TRAB NA TRAT SIO ZA SERIKALI

10 Nov, 2023
FEDHA ZILIZOPO KWENYE MASHAURI TRAB NA TRAT SIO ZA SERIKALI

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma kuhusu muda ambao Serikali itamaliza mashauri ya kikodi yaliyopo Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) ili fedha zilizopo huko zirudi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kufanyakazi za maendeleo na pia kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara.

 

Serikali imesema inajenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara kwa kutotumia fedha zilizopo kwenye mashauri yanayobishaniwa katika Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) ili kutoa haki kupitia vyombo hivyo vinavyoongozwa na Wanasheria mahiri.

Hayo yalielezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalam, Mhe. Janejelly James, aliyetaka kujua muda ambao Serikali itamaliza mashauri ya kikodi yaliyopo TRAT na TRAB ili fedha zilizopo huko zirudi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kufanyakazi za maendeleo na pia kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara.

Mhe. Dkt. Nchemba, alisema kuwa Fedha zinazobishaniwa na kabla hazijaamuriwa na vyombo husika haziwi fedha za Serikali hivyo haziwezi kutumiwa na Serikali katika shughuli zake za maendeleo.

“Serikali ingekuwa inyoosha tu mkono na kusema tunachokadiria sisi ndicho tunataka kilipwe! hiyo ndiyo ingeharibu mahusiano na walipa kodi. Fedha zilizopo TRAB na TRAT zitakuwa fedha za Serikali iwapo vyombo hivyo vitasema sasa hii ni fedha ya Serikali, hilo linafanyika ili kutoa fursa ya haki kutendeka”, alisema Dkt. Nchemba

Alisema kuwa hadi Oktoba 2023, Bodi ya Rufani za Kodi ilikuwa na mashauri 889 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi trilioni 6.46 na Dola za Kimarekani milioni 4.66 ambapo katika kipindi hicho, Bodi imesikiliza mashauri 167 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi trilioni 2.66 na Dola za Kimarekani 201,242.51.

Dkt. Nchemba alieleza kuwa Baraza la Rufani za Kodi lilikuwa na mashauri 176 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi bilioni 266.94 ambapo mashauri 91 yenye kiasi cha kodi kinachobishaniwa cha shilingi bilioni 166.32 yamesikilizwa.

Alibainisha kuwa katika mwaka 2023/24 TRAB na TRAT zinaendelea kutekeleza mpango maalum yaani “Special Sessions” ambapo kuanzia mwezi Novemba, 2023 hadi mwezi Juni, 2024 watasikiliza na kumaliza mashauri ya kodi yaliyofunguliwa.

Dkt. Nchemba alisema kuwa kupitia mpango huo, mashauri mengi zaidi yatasikilizwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuzingatia uwingi wa mashauri hayo, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, Ruvuma, Tabora, Mara, Manyara, Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe.

Mhe. Dkt. Nchemba alisema Serikali pia imeanzisha Taasisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Tax Ombudsman) ambayo jukumu lake kubwa ni kupokea malalamiko na kutatua masuala ya kikodi yanayotokana na huduma, hatua za kikodi na utekelezaji wa sheria za kikodi kati ya Mlipakodi dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Mwisho.