Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

ELIMU YA FEDHA NA TEKNOLOJIA KUCHOCHEA UJUMUISHAJI WA KIFEDHA

19 Nov, 2026
ELIMU YA FEDHA NA TEKNOLOJIA KUCHOCHEA UJUMUISHAJI WA KIFEDHA

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akizindua ripoti ya tathmini ya hali ya ujumuishaji wa kifedha kidigitali kwa wanawake na vijana wafanyabiashara nchini, wakati wa Mkutano wa Kilele wa Ujumuishaji wa Kifedha kwa Wanawake na Vijana, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

 

Elimu ya fedha inayoambatana na teknolojia pamoja na upatikanaji wa mitaji na gharama nafuu za huduma za kifedha ni maeneo muhimu yatakayochochea ujumuishaji wa kifedha kwa wanawake na vijana nchini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, wakati wa Mkutano wa Kilele wa Ujumuishaji wa Kifedha kwa Wanawake na Vijana uliofanyika Serena Hotel, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Luswetula amesema kuwa  elimu ya fedha itawawezesha wananchi kupanga matumizi, kuweka akiba na kukopa kulingana na uwezo wao, huku teknolojia za kidijitali zikisaidia kuwafikia wananchi ambao hawajafikiwa na huduma za kawaida za kifedha.

Kuhusu mitaji, Mhe. Luswetula amesema ukosefu wa dhamana ni kikwazo kikubwa kwa wajasiriamali wadogo kupata mikopo rasmi, hivyo kuzitaka taasisi za fedha kubuni bidhaa zinazozingatia hali halisi ya biashara za wanawake na vijana, ikiwemo kutumia historia ya miamala na mtiririko wa fedha katika kutathmini uwezo wa kukopa.

“Huduma za kifedha zinapaswa kuwa na gharama zinazomudu wananchi, kupitia ushindani wa haki, uwazi wa riba na ada, ulinzi wa watumiaji na kuimarisha mwingiliano wa mifumo ya malipo”, amesema Mhe. Luswetula.

Amesema kuwa Teknolojia iwe daraja la kupunguza pengo, si chanzo cha tofauti mpya, akihimiza watoa huduma kuhakikisha wanawake na vijana wanapata huduma za kidijitali kwa usalama na kwa kuzingatia faragha.

Aidha, ametoa wito kwa taasisi za fedha kuwaona wajasiriamali wadogo kama fursa ya kukuza biashara, ajira na uchumi wa Taifa, huku akiwahimiza wanawake na vijana kutumia mitaji kwa nidhamu, kuweka kumbukumbu sahihi za biashara na kuimarisha ujuzi wa kifedha.

Vile vile Mhe. Luswetula amesema kuwa  Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na wadau wengine kuchambua na kutekeleza mapendekezo ya utafiti uliozinduliwa katika mkutano huo, ili kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa huduma za kifedha.

Kwa upande wake rais wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), CPA. Mercy Sila, ameiomba Serikali na wadau wa sekta ya fedha kufanyia kazi mapendekezo yaliyotokana na tafiti kuhusu huduma za kifedha za kidijitali ili kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za kiuchumi na kukuza biashara zao nchini ikiwa ni pamoja na  wanawake na vijana kuhitaji fursa zilizo wazi na huduma zinazokidhi mahitaji yao halisi na wanazoweza kumudu.

Mapendekezo Mengine ni kuboresha mazingira ya upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha, kuhakikisha uwazi katika masharti ya mikopo kwa kuweka bayana viwango vya riba, ada na tozo kwa lugha rahisi pamoja na kuimarisha ulinzi wa wakopaji kwa kuweka mifumo rahisi ya kuwasilisha malalamiko na kuchukua hatua dhidi ya wakopeshaji wa kidijitali wasiosajiliwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Dkt. Mwajuma Hamza ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali zinazochangia kukuza ujumuishaji wa kifedha kidijitali nchini, akisema maendeleo hayo yameongeza fursa kwa wanawake na vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi na biashara.

Akizungumza kuhusu matokeo ya utafiti uliofanyika kutathmini ujumuishaji wa kifedha kidijitali, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya mifumo ya kidijitali, hususan katika huduma za kutuma na kupokea fedha pamoja na kufanya miamala ya kifedha. 

Mwisho.