Category Title

 • Government Budget Speeches
 • Ministry's Budget Speeches
 • Budget Books 2023/2024
 • Budget Books 2022/2023
 • Budget Books 2021/2022
 • Budget Books 2020
 • Budget Books 2018/2019
 • Budget Books 2015/2016
 • Budget Books 2014/2015
 • Content not found
 • Content not found
 • Content not found

ELIMU YA FEDHA KUFUNGUA FURSA ZA UKUAJI WA UCHUMI

16 Nov, 2023
ELIMU YA FEDHA KUFUNGUA FURSA ZA UKUAJI WA UCHUMI

Kamishna wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, akieleza umuhimu wa elimu ya fedha katika kukuza uchumi wakati wa mkutano na waandishi wa Habari ulioangazia Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa, uliofanyika jijini Dodoma.

 

Serikali imekusudia kuhakikisha wananchi wengi wanapata uelewa wa masuala ya fedha ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika huduma rasmi za fedha na kuongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya tatu ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwa mwaka 2023 yanayotarajiwa kufanyika jijini Arusha.

Dkt. Mwamwaja alisema Serikali inalengo la ifikapo mwaka 2025, takriban asilimia 80 ya wananchi watakuwa wamepata uelewa wa masuala ya fedha kwa kuwa wananchi wengi bado hawajafikiwa na elimu hiyo.

” Kutokana na Utafiti wa FinScope wa mwaka 2023 nchini, ni asilimia 53.8 tu ya nguvu kazi wanatumia huduma rasmi za fedha ambapo kundi kubwa la Watanzania halifaidiki na huduma hizo hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zingewawezesha kuchangia katika kukuza Pato la Taifa”, alibainisha Dkt. Mwamwaja.

Alisema kupitia Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, wananchi watajengewa uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini.

Dkt. Mwamwaja aliongeza kuwa elimu itakayotolewa itawawezesha wananchi kusimamia vizuri rasilimali fedha ikiwa ni pamoja na kuimarisha utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa na njia sahihi za kulipa madeni.

”Maadhimisho haya yanalenga kuwaunganisha wananchi, wajasiriamali na wadau wengine ili waweze kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta ya fedha katika kukuza na kuimarisha biashara zao”, alisema Dkt. Mwamwaja

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, alisema Sekta ya fedha ipo rasmi hivyo wananchi wanapopata huduma za fedha wahakikishe wanapata kutoka katika taasisi inayosimamiwa kisheria.

Aidha aliwakaribisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo yatakayofanyika katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid kuanzia tarehe 20 hadi 26 Novemba, 2023-jijini Arusha ili kupata elimu hiyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 – 2029/30, ambapo kwa mwaka huu yanaadhimishwa kwa kaulimbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi’’

Wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wanaotarajia kushiriki katika maadhimisho hayo ni pamoja na Wizara, Idara na Wakala wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi - Zanzibar, Wasimamizi wa Sekta ya Fedha, Taasisi za Fedha, Asasi zisizo za Kiserikali, Sekta Binafsi, Bodi za Wataalamu, Vyama vya Wafanyakazi, Vyombo vya Habari, Taasisi za Elimu na Utafiti, Washirika wa Maendeleo, Vyama Vilele vya Sekta ya Fedha, Makundi ya Watoaji wa huduma za fedha na Taasisi za Dini zinazotoa huduma hizo.

Mwisho.