Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

DKT. NCHEMBA: TANZANIA YAUNGA MKONO MKAKATI WA IMF WA KUSAIDIA MASUALA YA KIJINSIA

24 Jan, 2023
DKT. NCHEMBA: TANZANIA YAUNGA MKONO MKAKATI WA IMF WA KUSAIDIA MASUALA YA KIJINSIA
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa Tanzania inaunga mkono mpango ulioanzishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) la kuingiza masuala ya kijinsia kwenye utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.
 
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa majadiliano kuhusu mkakati wa Shirika hilo wa kuingiza masuala ya kijinsia kwenye mipango yake, uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
 
Amesema kuwa kwa upande wa Tanzania, Serikali itaendelea kutilia mkazo masuala hayo ya kijinsia kwa kuwekeza rasilimali fedha katika kuboresha afya ya mama na mtoto, utoaji elimu bila ada, na kuwawezesha wanawake kiuchumi.
 
Dkt. Nchemba ameiomba jumuiya ya kimataifa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha masuala hayo na kusifu ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na IMF ambapo ushirikiano huo umelenga katika maeneo matatu ikiwemo kuelekeza bajeti kubwa kwenye maendeleo ya watu kwa kuboresha makusanyo ya ndani kupitia kodi, kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na  kuimarisha usimamizi na matumizi ya fedha za Umma.
 
Alisema kuwa maendeleo ya kijamii katika sekta ya fedha na kuimarika kwa uchumi katika miaka ya hivi karibuni kumechangia kuongezeka kwa miaka ya kuishi kwa watanzania, kupungua kwa vifo wa watoto chini ya umri wa miaka mitano, kupungua kwa udumavu pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa jinsi zote wanaojiunga na masomo kwenye shule za msingi.
 
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Kituo cha Shirika la Fedha la Kimataifa Mashariki (AFRITAC), Bi. Li Xiangming, alisema kuwa Uamuzi wa Shirika lake wa kuingiza masuala ya kijinsia kwenye mipango yake umelenga kujenga jamii yenye usawa na kuwawezesha wanawake kushiriki katika kujenga uchumi na kupata maendeleo endelevu.
 
Alitaja baadhi ya maeneo yatakayotiliwa mkazo zaidi katika mkakati huo kuwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi, kumiliki ardhi, kupata elimu bora na kupiga vita aina zote za ukatili wa kijinsia zinazokwamisha maendeleo ya mwanamke na mtoto.
 
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi na Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa, Bw. Zlatan Milisic, aliipongeza Tanzania kwa kusimamia uchumi wake vizuri licha ya kuwepo kwa changamoto za Uviko 19 panoja na vita vinavyoendelea baina ya Urusi na Ukraine.
 
Aliahidi kuwa IMF kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa wataongeza jitihada katika kuiwezesha Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo ya milenia katika masuala mbalimbali ikiwemo kuwawezesha wanawake kiuchumi ili kujenga jamii iliyobora na jumuishi kiuchumi na kijamii.
 
Mkutano huo wa majadiliano kuhusu mkakati wa IMF wa kuingiza masuala ya kijinsia katika mipango yake umehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
 
Mwisho