Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

DKT.NCHEMBA: SEKTA BINAFSI ISHIRIKI KATIKA MIRADI

24 May, 2022
DKT.NCHEMBA: SEKTA BINAFSI ISHIRIKI KATIKA MIRADI

TAARIFA KWA UMMA

 

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, (Mb) ametoa rai kwa sekta binafsi nchini kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili kutoa nafasi kwa Serikali kutoa huduma kwenye maeneo ambayo sekta binafsi haiwezi kufika.

Alitoa rai hiyo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABSA Afrika, Bw. Saviour Chibiya ambaye Benki yake inamiliki zaidi ya asilimia 50 ya hisa za Benki ya NBC.

Alisema kuwa muelekeo wa Serikali ni kuwa kazi zinazoweza kufanywa na sekta binafsi ziweze kufanywa na sekta hiyo kwa sababu kadri sekta hiyo inavyokuwa ndivyo inavyotengeneza ajira kwa vijana.

“Sasa hivi Serikali inajenga Reli ya Kisasa lakini inakaribisha Sekta binafsi katika masuala ya uendeshaji na mengine yanayoweza kufanywa na sekta hiyo, mpaka sasa miongoni mwa mambo ambayo sekta binafsi imeshirikiana na Serikali katika suala hilo ni pamoja na kuleta vichwa vya treni na mabehewa jambo ambalo linatakiwa lifanyike katika sekta nyingine pia,’’ alisema Dkt. Nchemba.

Akieleza kuhusu sekta ya kilimo, Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali inatarajia kuanzisha miradi ya kilimo cha umwagiliaji na inatarajia kuona sekta binafsi hasa benki ikishiriki kikamilifu katika kuwawezesha wakulima hususani walio katika vikundi kwa kuwapa mikopo itakayowasaidia kupata mitaji ili waweze kuingia katika shughuli za uzalishaji.

Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Sekta zingine ambazo zinahitaji kwa kiasi kikubwa uwezeshaji kutoka sekta binafsi ni pamoja na uvuvi na ufugaji kwa kuwa ni maeneo ambayo yanaweza kuwa suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa  ajira kwa vijana.

Aidha, alipongeza benki hiyo kwa kuunga mkono sekta ya michezo kwa kudhamini ligi kuu ya Tanzania bara ambapo udhamini huo umechochea hamasa ya mchezo wa mpira wa miguu nchini.

Alitoa rai kwa benki hiyo kuendelea kuunga mkono Serikali katika sekta nyingine ikiwemo sekta ya afya ambapo, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, amejenga vituo vingi vya afya ambavyo vinahitaji vifaa tiba.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABSA Afrika, Bw. Saviour Chibiya, aliipongeza Serikali kwa jitihada za kukuza uchumi licha ya changamoto ya Uviko 19 pamoja na vita ya Urusi na Ukraine, jambo ambalo alilitaja kuwa ni kichocheo kikubwa cha uwekezaji.

Alisema kuimarika kwa uchumi kunawafanya wawekezaji ikiwemo Benki ya ABSA Afrika kuvutiwa kuwekeza Tanzania, hivyo benki yake ipotayari kuendelea kuwekeza nchini ili kuchochea maendeleo ya jamii kwa kuwa uwekezaji ni miongoni mwa jukumu lao muhimu.

Imetolewa na:

Benny Mwaipaja

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha ya Mipango