Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

DKT. MWAMBA: TUMIENI JUKWAA LA WANAWAKE NA KODI KUTOA ELIMU

17 Mar, 2026
DKT. MWAMBA: TUMIENI JUKWAA LA WANAWAKE NA KODI KUTOA ELIMU

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amewapongeza wanawake wanaofanya kazi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mchango wao mkubwa katika kusimamia na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, akisisitiza kuwa mapato hayo ndiyo msingi wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.


Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Dkt. Natu Mwamba alisema kuwa wanawake wameendelea kuwa na nafasi muhimu katika utumishi wa umma na katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.


Alisema maadhimisho hayo siyo tu ya kusherehekea fahari ya kuwa mwanamke bali pia ni fursa ya kukumbushana wajibu na majukumu ya wanawake katika familia, taasisi na Taifa kwa ujumla.


“Nawapongeza wanawake wote wa TRA kwa mchango wenu mkubwa katika kusimamia na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, ambayo ndiyo mhimili wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa letu,” alisema Dkt. Mwamba.


Dkt. Mwamba alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kusimamia sera na mifumo inayolinda na kukuza haki, usawa na ustawi wa wanawake katika sekta mbalimbali.


Alieleza kuwa katika Utumishi wa Umma zipo sheria, kanuni na miongozo inayolinda haki za wanawake, ikiwemo Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na marejeo yake, Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 pamoja na Standing Orders za mwaka 2009.


Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, miongoni mwa haki hizo ni pamoja na mtumishi mwanamke kupata siku 84 za likizo ya uzazi anapojifungua mtoto mmoja na siku 98 anapojifungua watoto zaidi ya mmoja, pamoja na haki ya kupata muda wa kunyonyesha mtoto hadi atakapofikisha miezi tisa.


Alisema haki hizo si upendeleo bali ni uwekezaji katika afya, ustawi wa familia na maendeleo ya Taifa.


“Mwanamke anapowezeshwa, taasisi inakuwa imara zaidi; na taasisi inapokuwa imara, Taifa linakuwa imara,” alisisitiza.


Aidha, aliwataka wanawake wa TRA kuendelea kuwa walinzi wa taswira nzuri ya taasisi hiyo kwa kuzingatia uadilifu, weledi, uwajibikaji na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kikazi.


Katika hatua nyingine, Dkt. Mwamba aliwapongeza wanawake wafanyabiashara na viongozi wa kampuni binafsi waliotunukiwa tuzo kwa kuwa walipakodi wazuri, akisema hatua hiyo ni mfano bora wa uzalendo na uwajibikaji.


Alisema ulipaji kodi kwa hiari unaonyesha uelewa, imani kwa Serikali na utayari wa kushiriki katika ujenzi wa Taifa, huku akibainisha kuwa kupitia kodi zinazokusanywa na TRA, Serikali imefanikiwa kugharamia miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta za afya, elimu, miundombinu na huduma za kijamii.


Dkt. Mwamba alisisitiza kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kuiwezesha TRA kuwa na mazingira ya kazi jumuishi na salama yanayowezesha wanawake kufikia ndoto zao na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.


Pia aliwahimiza wanawake wa TRA kutumia jukwaa la Wanawake na Kodi lililozinduliwa Machi 6, 2026 kuendelea kutoa elimu kwa walipakodi, hususan wanawake wajasiriamali, kuhusu umuhimu wa kujisajili, kutoa taarifa sahihi na kulipa kodi kwa wakati.


Alisema hatua hiyo itasaidia kujenga mazingira rafiki ya kodi yanayochochea ulipaji kodi kwa hiari na kuchangia ukuaji wa uchumi jumuishi nchini.

MWISHO