Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

DKT. MWAMBA: TANZANIA KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KATIKA MIUNDOMBINU AFRIKA.

06 Aug, 2026
DKT. MWAMBA: TANZANIA KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KATIKA MIUNDOMBINU AFRIKA.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza wakati wa hafla ya Chakula cha Usiku (Gala Dinner) iliyoandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa washiriki wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), iliyofanyika katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na wadau wa maendeleo pamoja na wawekezaji ili kuchochea maendeleo ya miundombinu barani Afrika.

 

Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na wadau wa maendeleo pamoja na wawekezaji ili kuchochea maendeleo ya miundombinu barani Afrika.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, wakati wa hafla ya Chakula cha Usiku (Gala Dinner) iliyoandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa washiriki wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), iliyofanyika katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mwamba alieleza kuwa, ushirikiano kati ya Tanzania, na wadau wa maendeleo ikiwemo Taasisi ya Africa50, umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uwekezaji wa miundombinu, huku akibainisha kuwa uchaguzi wa Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaonesha imani kubwa ya kimataifa kwa Tanzania kama kitovu cha uwekezaji na maendeleo barani Afrika.

“Pamoja na majadiliano ya kitaalamu yanayoendelea katika mikutano hii, hafla hii ya jioni imelenga pia kuimarisha mahusiano, kujenga urafiki na kuendeleza mtandao wa kitaaluma miongoni mwa washiriki lakini pia kwetu ni heshima kubwa kwa kuwa mwenyeji wa mikutano hii muhimu wa kimataifa” alisema Dkt. Mwamba.

Akizungumzia utamaduni wa Tanzania, Dkt. Mwamba alisema Tanzania ina zaidi ya makabila 120 yanayoishi kwa amani na mshikamano, hali inayochangia kuimarisha utulivu na kuvutia wawekezaji.

“Tunajivunia kushiriki nanyi sehemu ya urithi wetu wa kiutamaduni kupitia burudani, muziki na vyakula vya asili vitakavyowasilishwa usiku huu, utamaduni huu unaifanya Tanzania kuwa Taifa lenye ukarimu na linaloheshimu utofauti” alisema Dkt. Mwamba.

Aidha, aliwahimiza wageni kufurahia ukarimu wa Tanzania na kutumia fursa hiyo kuendeleza mazungumzo yatakayochochea ubunifu wa miradi ya miundombinu itakayobadilisha maisha ya Waafrika.

Alihitimisha kwa kuwashukuru washiriki wote kwa kuhudhuria mkutano huo na kuchangia mafanikio yake, huku akiwakaribisha kuendelea kufurahia uzuri na utajiri wa Tanzania.

“Karibuni Tanzania, karibuni sana,” alisisitiza Dkt. Mwamba.

Tukio hilo lilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb,) Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) na Mhe, Laurent Luswetula (Mb), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika -AfDB na Mwenyekiti wa Africa50, Dkt. Sidi Ould Tah, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Africa 50, Bw. Alain Ebobissé, na wageni mbalimbali wanaoshiriki Mkutano huo kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika.

MWISHO