Category Title

 • Government Budget Speeches
 • Ministry's Budget Speeches
 • Budget Books 2024/2025
 • Budget Books 2023/2024
 • Budget Books 2022/2023
 • Budget Books 2021/2022
 • Budget Books 2020
 • Budget Books 2018/2019
 • Budget Books 2015/2016
 • Budget Books 2014/2015
 • Content not found
 • Content not found
 • Content not found

CHUO CHA IAA CHATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU

07 Oct, 2022
CHUO CHA IAA CHATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimetakiwa kuongeza ubunifu katika utendaji kazi wake ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani yatakayowezesha Chuo hicho kujiendesha kikamilifu kwa kutumia mapato hayo.

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, wakati wa ziara yake katika Chuo hicho ambapo alitembelea miradi inayotekelezwa pamoja na kuzungumza na Menejimenti ya Chuo hicho, jijini Arusha.

Bi. Omolo alisema kuwa kuongeza ubunifu kutawezesha mapato ya ndani kuongezeka kwa kuwa changamoto zinapojitokeza zitaweza kutatuliwa kwa ushirikiano na kuibua mbinu mpya za kuongeza mapato.

‘’Kwenye kujiendesha lazima tuwe na timu ambayo inatengeneza ubunifu, ikiwa tumekupa chuo kwa miaka mitano unapotoka unatuachia nini, hakuna mtu mwingine atakuja kukutengenezea lakini ili mfanye vizuri lazima kuimarisha utawala bora,’’ alisema Bi. Omolo.

Alisisitiza kuwa ili kuweza kufanikiwa katika kuongeza mapato lazima Chuo kijenge jina na kuongeza sifa kwa kuhakikisha kuwa kinazingatia ubora wa elimu inayotolewa ili kuvutia wanafunzi wengi zaidi na pia kuwa na wahitimu watakaoweza kushindana katika soko la ajira kitaifa na kimataifa.

Aidha, Bi. Omolo, aliitaka Menejimenti ya Chuo hicho kuimarisha ushirikiano katika taasisi hiyo na kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali chuoni hapo unafanyika kwa ushirikiano na kutafuta mbinu za kutatua changamoto zinapojitokeza mapema kwa pamoja.

Alisema kuwa ameridhishwa na miradi ya ujenzi inayotekelezwa chuoni hapo na kuwasisitiza kila mmoja kuwa na taarifa za miradi hiyo ili kuwa na uelewa wa pamoja na kuhakikisha kuwa Taasisi inaweza kuendelea na shughuli zake bila kukwama.

Bi. Omolo aliongeza kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushirikiana na Chuo hicho ili kiweze kufanikisha malengo na mipango ya muda mrefu kwa kukiwezesha kifedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kuendeleza Chuo.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Cairo Mwaitete, aliishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano na kukiwezesha Chuo hicho katika kutimiza majukumu yake pamoja na kukipatia ruzuku ya Sh. bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, Kampasi ya Babati na kutoa kibali cha kukopa Sh. bilioni nane, kwa ajili ya ujenzi wa hosteli.

Akizungumzia mafanikio ha Chuo hicho, Dkt. Cairo Mwaitete, alisema kuwa Chuo kimeboresha uwezo wake wa kukusanya mapato yake ya ndani kutoka kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 6.4 kwa mwaka 2019/20 hadi kufikia Sh. bilioni 15.65 kwa mwaka wa fedha 2021/22.

‘’Chuo kimefanya jitihada za kujitangaza na kufanikisha kuongezeka kwa wanafunzi kwa miaka mitatu mfululizo kutoka wanafunzi 4,769 ambapo kufikia June 2022 Chuo kilikuwa na wanafunzi 10,342 na matarajio kwa mwaka wa masomo 2022/2023 ni kufikia wanafunzi zaidi ya 12,080’’, alisema Dkt. Cairo Mwaitete.

Alisisitiza kuwa Chuo hicho kitaendelea kutekeleza majukumu yake kufanikisha na kutimiza maono ya Serikali ya kuwezesha Taifa kupata nguvu kazi itakayokubalika kwenye soko la ajira kimataifa na kutoa mchango katika utatuzi wa changamoto za kijamii na kiuchumi kupitia tafiti na ushauri wa kitaalam.

 Mwisho.