Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

BENKI YA DUNIA YAAHIDI KUTOA DOLA MILIONI 300 AWAMU YA TATU TASAF

07 Dec, 2024
BENKI YA DUNIA YAAHIDI KUTOA DOLA MILIONI 300 AWAMU YA TATU TASAF
Benki ya Dunia imeahidi kutoa kiasi cha takribani Dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya kusaidia Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) ambayo inatajiwa kutekelezwa baada ya kukamilika kwa Awamu ya Pili ya Mpango huo mwakani.
 
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Bw. Nathan Belete katika Mjadiliano ya Ngazi ya Juu kati ya Serikali na wadau wa maendeleo kuhusu mustakabali wa Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF).
 
Bw. Belete alisema wameamua kutoa fedha hizo kwakuwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unatekelezwa na TASAF ni mfano wa kuigwa duniani kwasababu umechangia kukabiliana na umaskini na kuonesha matokeo chanya . 
 
Aliipongeza Serikali kwa mafanikio mbalimbali iliyoyapata kupitia Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini chini ya TASAF na kuahidi kuwa benki hiyo kwa kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha inafikia malengo yake hususan ya kuwawezesha wananchi kukabiliana na umaskini.
 
Naye Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ambaye aliongoza majadiliano hayo, alisema Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini itakuwa na mpango jumuishi utakao endana na Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoandaliwa ya 2025 -2050.
 
Alisema utakuwa mpango jumuishi kwa kuwa hatuo acha mtu yoyote nyuma kwa kuhakikisha kuwa unawezesha wananchi wa hali ya chini kujumuishwa katika mpango mkuu kwa kushiriki katika miradi mbalimbali inayoendelea nchini.
 
“Uandaaji wa Mpango wa Tatu wa TASAF utahusisha shughuli za uzalishaji ambazo hazita bagua sehemu ya jamii yetu, makundi yote yatahusishwa katika shughuli za maendeleo na mgawanyo wa bajeti kwa ajili ya maendeleo hayo ”, alisema Dkt. Nchemba.
 
Alisema Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini inaandaliwa baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Mpango wa Kwanza na Wapili  ambapo kumekuwa na shuhuda mbalimbali kutoka kwa wanufaika ambao vipato vyao vimeongezeka kutoka hatua moja kwenda nyengine kwa kuoonesha shughuli walizo fanikiwa kuzifanya kutokana na mradi huo.
 
Akizungumzia uchumi wa nchi, Dkt. Nchemba alisema uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.4 mwaka 2024 kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023 na kubainisha kuwa utendaji wa uchumi wa Tanzania kuanzia 2020 hadi 2024 unaonesha kuimarika. 
 
Alisema kukua na kuimarika huko kwa uchumi wa nchi kunatona na mabadiliko ya sera za Serikali na jitihada za kukabiliana na changamoto za kitaifa na kimataifa ambazo ni zimekuwa kikwazo cha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwan Kikwete alisema majadiliano hayo yamefanyika kwa kuwa Mpango wa Pili wa Kunusuru Kaya Maskini unatarajia kumaliza muda wake mwakani hivyo ilikuwa ni muhimu Serikali na wadau kukutana kuangalia namna bora ya kuanzisha Mpango mwengine ambao utakuwa na manufaa kwa Taifa. 
 
Alisema katika majadiliano hayo wadau wote muhimu wameonesha nia ya kuendelea kushirikiana na Serikali katika Mpango wa Tatu wa Kunusuru Kaya Maskini. 
 
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango - Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salim alisema ni muhimu Awamu mpya ya Kunusuru Kaya Masikini ifungamanishwe na masuala ya kidigitali ambayo yatawezesha wanufaika kupokea fedha kidigitali ili kuongeza usalama na kuhamasisha uwekaji akiba. 
 
Alisema Zanzibar pia ni wanufaika wa Mfuko TASAF ambapo wananchi wengi wanaoishi katika kaya maskini wamekuwa wakipatiwa misaada mbalimbali kupitia miradi ya Kunusuru Kaya Maskini.
 
Aliongeza kuwa licha ya miradi ya TASAF kusaidia kaya maskini kujiinua kiuchumi visiwani Zanzibar pia imesaidia kujenga shule na vituo vya afya. 
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray alisema kuwa Mpango wa Tatu wa Kunusuru Kaya Maskini unatarajia kugharimu takribani Dola za Marekani milioni 500 na kuhususha wanufaika wapya na baadhi ya wanufaika wa Awamu ya Pili ambao bado wahitaji msaada wakiwemo wazee wasiojiweza, wajane na wote watakao bainika kuwa halizao zinahitaji haziridhishi. 
 
Majadiliano hayo yalihusisha Mawaziri mbalimbali wa kisekta kutoka Tanzania Bara na Visiwani, Benki ya Dunia na wadau wa maendeleo nchini.