Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

BARA LA AFRIKA LIWEKE MIKAKATI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA VITA MASHARIKI YA KATI

04 Apr, 2026
BARA LA AFRIKA LIWEKE MIKAKATI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA VITA MASHARIKI YA KATI
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akichangia mjadala kufuatia taarifa ya Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Uchumi Afrika (UNECA), iliyochambua athari za mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati namna ulivyoleta athari hasi za kiuchumi na kijamii katika Bara la Afrika na namna ya kukabiliana nazo, katika Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi na Magavana wa Benki Kuu wa Afrika, unaofanyika jijini Tangier nchini Morocco.
 
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ametoa wito kwa nchi za Afrika kuwa na mtazamo wa pamoja katika kubuni na kutekeleza mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu, ambayo ni endelevu na jumuishi, itakayopunguza utegemezi na kuimarisha
uthabiti wa uchumi wa Bara la Afrika ili kukabiliana na majanga na migogoro ya vita inayoendelea duniani.
Mhe. Balozi Omar alitoa wito huo jijini Tangier nchini Morocco, katika Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi na Magavana wa Benki Kuu wa Afrika, wakati akichangia mjadala kufuatia taarifa ya Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Uchumi Afrika (UNECA), inayochambua athari za mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati namna ulivyoleta athari hasi za kiuchumi na kijamii katika Bara la Afrika.
Alibainisha kuwa baadhi ya nchi za Afrika, hususan zile zinazotegemea sekta ya utalii, zinaweza kuathirika zaidi na Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
Kwa upande wa Tanzania, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mgogoro huo kupitia ushirikiano katika Wizara za Kisekta na Taasisi zake, ili kubaini hatua stahiki za kisera zitakazolinda ustawi wa uchumi na maslahi ya wananchi.
Vilivile, alieleza kuwa pamoja na kwamba mgogoro huo umeathiri mtiririko wa biashara kwa kuwa ukanda wa Mashariki ya Kati ni lango muhimu la biashara kati ya Afrika na masoko ya kimataifa. Hivyo, ni muda muafaka wa Afrika kuona umuhimu wa kuwa na njia mbadala ya kufanya biashara hususan miongoni mwa nchi wanachama.
Mheshimiwa Balozi Omar alisisitiza kuwa kwa muda mrefu Afrika imekuwa ikijadili umuhimu wa kutumia rasilimali zake ipasavyo, na kwamba hali ya sasa inatoa fursa ya kuchukua hatua madhubuti za kujitegemea kwa kutumia rasilimali zake.
Alifafanua kuwa Bara la Afrika lina rasilimali za kutosha, ikiwemo mafuta na mbolea, ambazo zinaweza kuzalishwa na kupatikana ndani ya Bara kupitia ushirikiano, hususan Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Mhe. Balozi Omar alieleza kuhusu umuhimu wa kuendelea na majadiliano chini ya uratibu wa UNECA kuhusu mageuzi katika mifumo inayosimamia maamuzi na sera za kifedha duniani (Global Financial Architecture), ili Afrika iweze kuwa na sauti moja yenye nguvu katika upatikanaji wa rasilimali za kifedha kwa gharama nafuu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya mageuzi hayo yatategemea mshikamano na ushirikiano thabiti wa nchi za Afrika.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo, walieleza kuwa ili kukabiliana na mizozo hiyo nchi za Afrika zinahitaji kuweka sera na mikakati ya kuondoa vikwazo vya ufanyaji biashara na upitishaji wa bidhaa kwa kufungua mipaka yake.
Aidha, walishauri kuwa umefika wakati wa nchi za Afrika kuzalisha mafuta yake na kutumia vyanzo vingine mbadala vya nishati ili kukabiliana na uhaba wa mafuta na kupanda kwa bidhaa hiyo muhimu katika uzalishaji na uchumi wa mataifa hayo.