Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

BALOZI OMAR: MAGEUZI YA UCHUMI KUCHANGIA USTAWI WA WANANCHI

05 Feb, 2026
BALOZI OMAR: MAGEUZI YA UCHUMI KUCHANGIA USTAWI WA WANANCHI

Waziri wa Fedha, Mhe Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) akieleza kuhusu maeneo ya uwekezaji wakati wa mkutano na  Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa ya Moody’s Investor Service, ikiongozwa na  Bw. John Walsh (hayupo pichani), kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

 

Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa mageuzi ya uchumi yataendelea kuwa ajenda ya muda mrefu yakilenga si tu kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi bali kuhakikisha ukuaji huo unachangia katika upatikanaji wa ajira na ustawi wa wananachi kwa ujumla.

Amebainisha hayo wakati wa kikao na Timu ya Wataalamu kutoka Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa ya Moody’s Investor Service ikiongozwa na  Bw. John Walsh, kilichofanyika Ofisi za Treasury Square, jijini Dodoma.

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa uchumi wa nchi umeendelea kuimarika licha ya matukio kadhaa yaliyokwaza ustawi wa uchumi wa dunia ukiwemo uviko 19 ambapo katika kipindi cha mwaka jana uchumi ulikua kwa asilimia 5.4 na unatarajiwa kukua zaidi mwaka huu wa fedha 2025/26 hadi kufikia asilimia 6.

Aidha, alibainisha kuwa mahitaji ya uwekezaji yanaendelea kuwa makubwa hususani kwenye miundombinu ya kimkakati kama Bandari, Viwanja vya Ndege, Reli na mtandao wa Barabara ili kuchochea maendeleo.

Alieleza kuwa nchi inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Reli iendayo Kasi -SGR, Bwawa la uzalishaji wa umeme la Julius Nyerere na uimarishaji wa sekta nyingine za kijamii na kiuchumi hatua itakayochochea zaidi ukuaji na uimara wa uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii.

Akizungumzia Mfumuko wa bei amesema kuwa, hali imeendelea kuwa tulivu ambapo kiwango cha mfumuko wa bei kimeendelea kubaki chini ya asilimia tano kwa miaka kadhaa, kikiwa kati ya asilimia 2.9 na 3.4.

Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa Moody’s,  Bw. John Walsh, alisema kuwa uamuzi wa kupandisha hadhi ya uwezo wa nchi kukopesheka na kuipa alama B1 yenye mtazamo thabiti ulitokana na uthabiti wa kiuchumi na kifedha ambao nchi imeuonesha licha ya changamoto za uchumi za dunia katika miaka ya karibuni.

Alisema kuwa Tanzania iliendelea kurekodi ukuaji thabiti wa uchumi licha ya athari za janga la UVIKO-19, mfumuko wa bei wa kimataifa na kupanda kwa viwango vya riba duniani.

“Uamuzi wa kupandisha hadhi kwa kiwango cha B1 ulitokana na uthabiti wa sera za uchumi jumla na mageuzi ya Serikali yanayotekelezwa chini ya Mpango wa Shirika la Fedha la Kimatafa (IMF), unaokaribia kukamilika”, alisema Bw. Walsh.

Alisema kuwa Serikali imepiga hatua muhimu katika kushughulikia changamoto za muda mrefu, ikiwemo ukusanyaji mdogo wa mapato ya ndani na mapungufu ya utekelezaji wa sera, hivyo Tathmini ya sasa inalenga kufuatilia mafanikio, changamoto zilizopo, na mwelekeo wa mageuzi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Aidha alieleza kuwa tathmini hiyo inalenga kupata taswira ya kina ya hali ya sasa ya uchumi wa Tanzania, mafanikio yaliyopatikana, pamoja na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha ukuaji endelevu na uthabiti wa kifedha kwa muda mrefu.

Matokeo ya mapitio ya hivi karibuni ya Kampuni za Moody’s na Fitch ziliipa Tanzania daraja la B1 (stable outlook) na B+ (stable outlook), mtawalia ambayo yanaonesha kwamba Tanzania ni nchi salama kwa wawekezaji.

Mwisho.