Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

BALOZI OMAR ATOA WITO WA KUREJESHA MAADILI MEMA KATIKA JAMII

22 Nov, 2026
BALOZI OMAR ATOA WITO WA KUREJESHA MAADILI MEMA KATIKA JAMII

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiagana na  Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir baada ya hafla ya ugawaji wa zawadi kwa washiriki na washindi wa mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) na Uzinduzi wa Huduma ya Daktari wangu kupitia Mfuko wa Bima ya Mufti,  iliyofanyika katika Msikiti wa BAKWATA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana katika kurejesha na kuimarisha maadili mema katika jamii, akisisitiza kuwa jukumu la kujenga jamii yenye maadili si la Serikali pekee, bali linawahusu wazazi, walezi, walimu, viongozi wa dini na kila mwanajamii.

Mhe. Omar ameyasema hayo wakati wa hafla ya ugawaji wa zawadi kwa washiriki na washindi wa mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa kupitia Kampeni ya Rudisha Maadili kwa Jamii na Uzinduzi wa Huduma ya Daktari wangu kupitia Mfuko wa Bima ya Mufti,  iliyofanyika katika Msikiti wa BAKWATA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Amesema suala la maadili ni jambo la msingi katika maendeleo ya jamii na linapaswa kuanzia katika familia, kuendelezwa shuleni, katika nyumba za ibada na maeneo mbalimbali ya kijamii.

“Hapo awali malezi ya watoto yalikuwa jukumu la pamoja la wazazi na jamii nzima, huku walimu na viongozi wa dini wakichangia katika kuwajenga watoto katika misingi ya heshima, nidhamu na uwajibikaji, kwa sasa kuna changamoto katika mfumo wa malezi, hali inayohitaji jamii kutafakari upya wajibu wake na kuchukua hatua za pamoja kurejesha utamaduni wa kulea watoto katika misingi ya maadili mema”, amesema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, ametoa pongezi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kusisitiza umuhimu wa maadili katika jamii.

Akizungumzia mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW), Mhe. Omar amesema mashindano hayo yamekuwa sehemu ya kutoa elimu kwa washiriki kuhusu maisha na mafundisho ya Mtume, huku akisisitiza kuwa lengo la elimu hiyo halipaswi kuishia katika kushiriki mashindano au kupata zawadi.

Amesema washindi waliopata zawadi wanastahili pongezi, lakini kwa maana pana, kila aliyeshiriki na kupata elimu kupitia mashindano hayo ni mshindi, kwa sababu mafanikio makubwa yatakuwa pale elimu hiyo itakapotumika katika maisha halisi.

Vilevile Mhe. Balozi Omar ametoa shukrani kwa waandaaji wa kampeni hiyo, washiriki na wadau wote waliofanikisha mashindano hayo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika kurejesha na kudumisha maadili mema kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania.

Kwa upande wake Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na jamii katika kuimarisha maadili na kuchochea maendeleo ya Watanzania.

Amesema ujenzi wa jamii yenye maadili mema unahitaji kila upande kutekeleza wajibu wake kwa kushirikiana, huku akibainisha kuwa maendeleo ya nchi yanapaswa kuzingatia maeneo muhimu ya elimu, uchumi, afya na ustawi wa jamii.

Sheikh Dkt. Zubeir ameeleza kuwa Serikali na wadau wengine wanapaswa kuendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi kupata elimu na huduma muhimu, pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Naye Meneja Mahusiano wa Taasisi ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Bi. Khadija Maulid, akizungumzia suala la Bima kwa wote, ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana na kuunga mkono Mfuko wa Bima ya Mufti katika kuhamasisha upatikanaji wa huduma za bima ya afya, hususan kwa wananchi wenye uhitaji.

Amesema ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya kupata huduma za matibabu bila kukabiliwa na changamoto kubwa za kifedha pale wanapougua.

Awali Mtoto Rehema Suleiman Kizenza aliyeibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (S.A.W), baada ya kuonesha umahiri na uelewa mkubwa kuhusu maisha, mwenendo na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W), alisema somo la Sira ya Mtume lina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku, hususan kwa watoto na wanafunzi, kwa kuwa linawafundisha maadili mema.

Alisema kujifunza Sira ya Mtume kunamsaidia yeye na wanafunzi wenzake kuwa waaminifu, wakweli, wenye huruma, wanyenyekevu na wenye kuzingatia adabu katika maisha yao ya kila siku.

 Mwisho.