Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

AICAD YATAKIWA KUENDELEA KUTUMIA TAFITI KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAENDELEO.

28 Sep, 2026
AICAD YATAKIWA KUENDELEA KUTUMIA TAFITI KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAENDELEO.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (kulia), akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya African Institute for Capacity Development (AICAD), Prof. James Njiru, baada ya mazungumzo kuhusu kuimarisha ushirikiano katika shughuli za ujenzi wa uwezo na maendeleo nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi yake, Treasury Square, jijini Dodoma.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ameitaka Taasisi ya African Institute for Capacity Development (AICAD) kuendelea kuimarisha matumizi ya tafiti, mafunzo na ushirikiano kati ya vyuo vikuu, sekta ya viwanda na jamii ili kupata suluhu za changamoto za maendeleo na kuchochea maendeleo endelevu katika nchi za  Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Dkt. Mwamba ametoa rai hiyo Ofisini kwake Treasury Square jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa AICAD ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Prof. James Njiru, kuhusu kuimarisha ushirikiano na shughuli za taasisi hiyo yenye makao makuu yake jijini Nairobi, Kenya.

Alisema AICAD ina mchango muhimu katika kujenga uwezo wa watu na taasisi kupitia utafiti bunifu, mafunzo na shughuli za kuwafikia wananchi, kwa lengo la kuchangia juhudi za kupunguza umaskini barani Afrika.

Alieleza kuwa taasisi hiyo, inayotekeleza shughuli zake nchini Tanzania, Kenya na Uganda, inashirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) nchini Tanzania, Makerere nchini Uganda na Egerton nchini Kenya katika kuendeleza utafiti, ubunifu na matumizi ya maarifa kutatua changamoto za jamii.

“Naipongeza AICAD kwa jitihada zake za kuhakikisha inaleta maendeleo katika nchi za Afrika kwa kuwa na mikakati imara na endelevu inayoonesha dhamira ya kuwasaidia wananchi kujikwamua kutoka katika umaskini, kupitia mafunzo na kujenga uwezo, hususan katika sekta ya kilimo,” amesema Dkt. Mwamba.

Aliitaka taasisi hiyo kuendelea kuunganisha taasisi za elimu ya juu, sekta ya viwanda na jamii ili kuhakikisha maarifa yanayozalishwa kupitia tafiti yanatumika kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AICAD, Prof. James Njiru, alisema taasisi hiyo inawezesha watafiti, wasomi na wadau mbalimbali kupata huduma na kutumia miundombinu ya utafiti, ikiwemo mifumo ya kompyuta, programu za kompyuta, maktaba, maabara na vifaa vingine vya kufanyia tafiti. 

Alisema upatikanaji wa rasilimali hizo unalenga kuongeza uwezo wa watafiti kufanya tafiti zenye tija, kuzalisha maarifa na kuandaa suluhu zinazoweza kutumika kukabiliana na changamoto za maendeleo.

Prof. Njiru alisisitiza kuwa AICAD inaendelea kuunganisha maarifa ya kitaaluma na mahitaji ya jamii kupitia utafiti, mafunzo na ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanakuwa na manufaa kwa wananchi.

Alisema kuwa uwekezaji katika ujenzi wa uwezo, upatikanaji wa rasilimali za utafiti na matumizi ya maarifa katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi ni miongoni mwa njia zinazoweza kuchangia kupunguza umaskini na kuimarisha maendeleo endelevu barani Afrika.

Mwisho.